Thursday, April 16, 2015

Wanafunzi WA KAMPALA INTERNATIONAL UNIVERSITY (KIU) kilichoko Gongo la Mboto wagoma



Wanafunzi WA KAMPALA INTERNATIONAL UNIVERSITY (KIU) kilichoko Gongo la Mboto wagoma
Wanafunzi  wa vitivo vya Sayansi ya Afya wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Kampala-tawi la Dar es Salaam (KIU), wamegoma kuendelea na masomo baada ya kubaini kuwa kozi wanazosoma katika chuo hicho hazijasajiliwa katika ya bodi mbalimbali kama taratibu na sheria zinazoelekeza.
Walianza mgomo huo tangu Ijumaa iliyopita baada ya kugundua kuwa kozi wanazofundishwa hazijasajiliwa katika Bodi ya Mafamasia, Bodi ya Maabara na Baraza na Madaktari. 
Walisema jana chuoni hapo kuwa wamekuwa wakiendelea na masomo bila kugundua kama kozi wanazochukua hazijasajiliwa katika bodi hiyo huku uongozi wa chuo ukikaa kimya.
Waziri wa Afya wa Serikali ya Wanafunzi (KIUSO), Kenedy Murunya, alisema walibaini kuwa kozi wanazosoma hazijasajiliwa baada ya kwenda katika ofisi za bodi na kuelezwa kuwa hazijasajiliwa. Wanafunzi waliokumbwa na tatizo hilo ni wale wanaochukua Shahada za maabara, udaktari na upasuaji.
"Wanafunzi walipokwenda Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) waliambiwa kuwa tume imeshafanya asilimia 50 ya usajili wa chuo hicho na asilimia 50 nyingine zilizobaki zinatakiwa zishughulikiwe na bodi husika za usajili," alisema.
Mwakilishi wa Kitivo cha udaktari (SUGA)), Martin Augustine, alisema 2013 wakati wanaanza masomo waliambiwa na uongozi wa chuo kuwa kozi zao zimesajiliwa bila kujua walikuwa wanadanganywa  na  uongozi  wa  chuo hicho.
Alisema mwaka huu walikwenda Bodi ya Madaktari Tanganyika wakaambiwa kuwa bado kozi yao haijasajaliwa kutokana na uongozi wa KIU kuzembea kutuma nakala muhimu zitakazofanikisha usajili.
Alisema Ijumaa baada ya mgomo wawakilishi wa vitivo vya sayansi wa ngazi zote za masomo walifanya kikao na uongozi wa chuo chini ya OCD wa Ilala kujadili matatizo ya usajili na uongozi na kuwa cha ajabu wawakilishi hao hawakupewa majibu yanayoridhisha hali iliyosababisha mgomo huo kuendelea.
Alisema tangu mgomo uanze Jeshi la Polisi limeweka kambi likiangalia hali ya usalama wa chuo. 
Alisema Septemba, 2014 walikwenda Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa lengo la kumuona Waziri, Dk. Shukuru Kawambwa, lakini hawakumuona hivyo kumwandikia  barua ili awape majibu ambayo hadi sasa hawajapatiwa.
Alisema wanaendelea kulipa ada kubwa japokuwa serikali ilikiagiza chuo hicho kushusha ada cha kushangaza Baraza la KIU ambalo lipo Uganda lilikataa maagizo ya serikali.
Alisema wanafunzi wa udaktari mwaka wa pili wanalipa Sh. milioni 8 wakati wa mwaka kwanza wanatozwa Sh. milioni 6.7, maabara sh. milioni 4.8, Famasia milioni 5.4 huku wa mwaka wakilipa sh. milioni 3.8.
Kwa mujibu wa Waziri Mkuu wa KIUSO, Elisha Mushi, mgomo huo unajumuisha wanafunzi wa vitivo vya sayansi pekee wakati vitivo vya biashara na sharia vinaendelea na masomo.
Hadi tunakwenda mitamboni, jitihada za  kumpata Rais wa KIUSO, Elias Mbogo pamoja na Waziri wa Elimu, Answari hazikufanikiwa baada ya kuambiwa kuwa wote wamekwenda Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kupata ufumbuzi wa matatizo ya wanafunzi.
Hata hivyo, Naibu Waziri wa Elimu wa Kiuso, Fadhilina Kassim, alisema anachofahamu yeye kuwa chuoni hapo kuna mgomo wa wanafunzi, lakini mwenye dhamana ya kuzungumzia suala hilo ni Waziri wa Elimu au Waziri Mkuu.
Afisa Masoko na Uhusiano wa KIU, Keneth Uki, alithibitisha kuwapo kwa mgomo wa wanafunzi hao huku akisisitiza kuwa vitivo vingine vya sayansi vimeshakamilika usajili ingawa kitivo cha wanafunzi wanaochukua Famasia tu ndio kozi zao hazijakamilisha usajili katika Baraza la Famasia Tanzania.
Wanafunzi hao wanaiomba wizara husika iwapatie ufafanuzi kuhusiana na suala hilo pamoja na uhalali wao KIU kwa kuwa walijiunga na chuo hicho kupitia TCU na NACTE.