Mtaa wa Mwatulole, wilayani Geita mkoani Geita, ndiko anakopatikana mtoto Saidi Idd , (so jina lake halisi), mwanafunzi wa darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Mwatulole mwenye umri wa miaka saba.
Ni mtoto anayeishi na wazazi wake lakini ndiye mtoto mkubwa kati ya watoto wanne anayetegemewa na wenzake.
Nafika nyumbani kwao nikiongozana na mtoto huyo, walimu wake na Ofisa wa Polisi Dawati la Jinsia.Tunapokelewa na mwanamke anayejitambulisha kuwa ni shangazi yake na Saidi.
Tulijitambulisha na kumhoji kama anafahamu jambo lolote juu ya tukio la ukatili alilofanyiwa mtoto huyo na mama yake mzazi, Mariam Hassan la kumchoma mkuki eneo la paji la uso na kumsababishia majeraha makubwa.
Mwanamke huyo anakataa kufahamu tukio hilo, kwa madai kuwa haishi nao isipokuwa alipigiwa simu na Mariam aje amlelee watoto kwani yeye (Mariam) anakwenda kufungwa.
Mara alituitia mdogo wake Saidi aliyekuwa ndani, alitoka lakini alionekana kuwa katika hali ya huzuni na aliyedhoofika.
Unyonge wa mtoto huyo uliashiria kuwa kuna jambo zito kwenye familia hiyo. Alitusalimia kwa adabu huku akijitambulisha kuwa anaitwa Amina Iddi (si jina lake halisi) mwenye umri wa miaka sita.
Aliingia ndani na kutuletea viti, tukaketi na kuanza kuzungumza na mtoto huyo, ambaye alionekana kuwa na siri nzito moyoni.
Alitusimulia mkasa wa kaka yake alivyochomwa mkuki Machi 26.
Asha anasema mdogo wake alikuwa anacheza na wenzake nje ya nyumba yao muda wa jioni, ghafla mama yao alifika na akamuuliza (Asha) alipo Said.
Anasema alimwita na alichukua mkuki ambao huwa anautunza ndani kwa ajili ya kuwapigia, akamchoma usoni, akaondoka kwenda kulala kwa sababu tu kaka yake hakufua nguo za shule.
"Aliondoka kwenda kulala bila hata kumwangalia kaka kama aliumia. Ila alikuwa anatokwa na damu, nikachukua maji nikamwagilizia ili kuzuia damu zisitoke na kumfunga nguo usoni. Damu zilikuwa zikimtoka sana," anasema Asha na kuongeza:
"Mama aliingia chumbani na kulala, wala hakujali kama tumekula, tulikwenda kulala baada ya kumfunga kaka nguo, asubuhi tukaamka kwenda shule wala hakutuaga."
Anasema wakati wanakwenda shule, kaka yake aliendelea kutokwa damu baada ya kufungua ile nguo aliyokuwa ameifunga kwenye jeraha.
Anasema yeye na kaka yake wanasoma shule na darasa moja, wakiwa darasani walikuja walimu wakamwona anatokwa na damu wakamwita ili awaeleza kilichomsibu kaka yake.
"Niliwaambia kuwa alichomwa mkuki na mama usiku, wakamwita mama akaja shuleni, polisi wakamkamata wakamchukua na kaka wakawapeleka hospitali," anasimulia Asha.
Anatoboa siri
Asha anasema mama yake alinunua panga na mkuki na kuuweka ndani kwa lengo la kuwapigia.
Anasema tukio la kaka yake kuchomwa na mkuki lilikuwa la kwanza. "Lakini mimi huwa akinifanyia hivyo mara kwa mara kwasababu hajanizaa yeye, mimi ni mtoto wa kambo.
"Na wakati mwingine huwa ananipiga na ubapa wa panga. Ametunza panga na mkuki ndani, huwa anatupiga kwa kutumia fimbo au ubapa wa panga, alishawahi kunipiga hapa…(anaonyesha majeraha ya ubapa wa panga)," anasema.
Anasema aliwahi kumtoboa na mkuki mkononi, pia mtoto huyo anasema yeye ndiye mpishi hasa baba yake asipokuwapo.
"Nafanya kazi zote za nyumbani, kuosha vyombo, kupika, kumlea mdogo wangu kufua nguo zetu na za mtoto," anaelezea.
Said anasimlia
Anasema mama yake amekuwa mkatili na hana upendo kwa watoto, kwasababu huwa anawapiga mara kwa mara tena kwa kutumia vitu vyenye ncha kali.
Mama mzazi anena
Mariam anakiri kumchoma mkuki mtoto wake, lakini anadai halikuwa kusudio lake bali ni bahati mbaya.
"Ni ajali tu sikuwa na wazo la kumchoma mwanangu, nilitoka msibani nimechoka nikakuta hajafua nguo ndiyo nikachukua mkuki kumpiga wakati najaribu kumchapa akajisogeza kwenye ncha ndiyo ukamchoma," anasema.
Anasema hakujua kama mkuki huo umemjeruhi kiasi hicho, hivyo alikwenda kulala na kuwaambia wapakue chakula wale.
"Nilishika mkuki akawa anataka kukimbia, nikamwambia nitakuchapa akawa analia sikujua kama aliumia kiasi hiki," anajitetea Mariam.
Mariam anakiri mtoto wake alipokwenda shule hakumwangalia wala kumkagua, kwani alikuwa amelala ila alishangaa kuwaona walimu na polisi wakija nyumbani kwake kumkamata.
Mwalimu anasemaje?
Mwalimu Catherine Matibijo aliyekuwa zamu, anasema asubuhi wakiwa mstarini akikagua wanafunzi, alishangaa kumwona mtoto huyo akitokwa na damu nyingi usoni.
"Nikamuuliza ilikuaje akaniambia alipigwa na mama yake mzazi usiku, nikamruhusu aingie darasani kwanza," anasema.
Alisema baadaye alienda kumwambia mwalimu wake wa darasa, Theresia Makelele, walimchukua na kwenda naye kwa mwalimu mkuu.
"Tukaanza kumhoji, akasema ana dada yake wanasoma darasa moja, tukamwita akatuelezea, tukampigia simu mama yao na kumwambia kuwa mtoto anaumwa sana," anasema Mwalimu Matibijo.
Anasema mama yake alitii na kufika, wakamuuliza na kukiri kutenda kosa hilo kwa majibu ya dharau, wakamwacha arejee nyumbani na wao wakaamua kutoa taarifa polisi.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya Geita, Adam Sijaona anakiri kumpokea mtoto huyo akiwa na majeraha eneo la usoni lililotokana na kuchomwa na kitu chenye ncha kali. "Tulimpokea mtoto huyo na tumemshona nyuzi sita, hali yake inaendelea vizuri," anasema Dk Sijaona.
Ofisa wa Polisi Dawati la Jinsia, Butono Kasusula anasema kosa alilolifanya Mariamu ni kinyume cha Sheria ya Mtoto kifungu Namba 21 ya mwaka 2009.