Thursday, April 16, 2015

MAAJABU 5 AJALI YA BASI NA FUSO



MAAJABU 5 AJALI YA BASI NA FUSO
Muonekano wa alama ya mnyama anayefanana na Chui akitembea akiwa na mtoto wakati wa magari hayo yakiwaka moto.
MAAJABU matano yameibuka kufuatia ajali mbaya iliyohusisha lori aina ya Fuso na basi la abiria iliyotokea Jumapili iliyopita eneo la Iyovi, Ruaha, Kilosa mkoani Morogoro ambapo zaidi ya watu 19 walifariki dunia, 13 kati yao kuteketea kwa moto na kuzikwa kwenye kaburi moja katika Makaburi ya Msavu mwanzoni mwa wiki hii.
Ajali hiyo ilitokea baada ya lori hilo lenye namba za usajili T 164 BKG kugongana na basi la abiria la Kampuni ya Nganga lenye namba za usajili T 373 DAH lililokuwa likisafiri kutoka Kilombero mkoani Morogoro kuelekea Mbeya eneo la Kijiji cha Msimba katika Tarafa ya Mikumi.
Picha ikionyesha mtu akiwa amevaa vazi la kanzu huku kiunoni kama  amejifunga mkanda, kama zilivyo picha za kuchorwa zinazowaonesha wanafunzi wa Yesu, Inasemwa na watu kuwa mtu huyo, huenda ni malaika wa amani.
Ajabu la kwanza linaloonekana kwenye picha zilizopigwa wakati magari hayo yakiungua moto, zinaonesha alama ya mnyama anayefanana na Chui akitembea akiwa na mtoto wake, kitu ambacho kimewafanya watu wengi kushindwa kutafsiri suala hilo.
Kana kwamba haitoshi, katika picha hiyo chini kidogo ya mnyama huyo, kuna ajabu lingine ambapo picha kama ya mtu akiwa amevaa vazi la kanzu huku kiunoni kama  amejifunga mkanda, kama zilivyo picha za kuchorwa zinazowaonesha wanafunzi wa Yesu. Inasemwa na watu kuwa mtu huyo, huenda ni malaika wa amani.
Ajabu la tatu katika tukio hilo la kusikitisha ni mpigapicha ambaye anahisiwa kuwa ndani ya gari dogo, umbali wa mita kadhaa kutoka eneo la tukio. Lakini wakati picha hiyo ikionesha mvua zilikuwa zikinyesha na barabara kuonekana kuloa kutokana na maji ya mvua, lakini katika eneo ambalo magari hayo yaligongana, kunaonekana kukavu jambo linalozua maswali mengi kuliko majibu.
Ajabu la nne ni kuwepo kwa taarifa kutoka kwa walionusurika katika ajali hiyo kuwa mmoja wa marehemu, aliweza kuzungumza kwa simu na wanaodhaniwa kuwa ndugu zake wakati akiteketea kwa moto. Inadaiwa kuwa walimsikia akiwaambia kuwa sauti wanayoisikia ni ya moto na kwamba atakata kauli wakati wowote na hakuelewa kama wangeitambua maiti yake.
Muonekano wa magari hayo baada ya kuwaka moto.
Na ajabu la mwisho kabisa katika ajali hiyo ni maelezo ya kuwa mmoja wa marehemu aliyefariki dunia baada ya kuungua moto, ni pale alipotambuliwa baada ya kuonekana mabaki ya mguu wake mmoja, uliokuwa na kiatu. Inadaiwa kuwa ndugu walimtambua kutokana na masalia ya kiatu hicho, ingawa mwili wake wote ulikuwa umeungua vibaya na asingeweza kutambuliwa.
Hata hivyo, akizungumza na gazeti hili kuhusu ajali hiyo, mtabiri maarufu Maalim Yahya Hussein, alisema ajali hiyo haikuwa ya kawaida, kwani siyo rahisi kwa moto kuanzia kwenye buti, tena kwa mlipuko wa ghafla. Aliihusisha ajali hiyo na harakati za kisiasa, akisema ni mwaka wa uchaguzi, ambao una mambo mengi.
Polisi wakiwa eneo la tukio.
Kuhusu picha ya mtu anayeonekana, ambaye katika mitandao kadhaa ya kijamii anatajwa kuwa ni malaika, alisema anayeonekana siyo malaika, kwani wao kazi yao ni kusaidia.
Mazishi ya watu hao yalifanyika Jumatatu iliyopita na kuhudhuriwa na viongozi wa dini zote, wa serikali na baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa, tukio hilo la simanzi lililowatoa machozi mamia ya waombolezaji waliojitokeza.