
Mwandishi wetu.
HALI ya mazingira nchini imeendelea kuwa mbaya ambapo zaidi ya hekari 400,000 za misitu hupotea kila mwaka huku matukio ya uchomaji moto ovyo yakiongezeka hadi kufikia 1,123,000 kwa kipindi cha mwaka 2000-2011.
Hayo yalibainishwa jana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Mhandisi Dk. Bilinith Mahenge, wakati wa uzinduzi wa ripoti ya pili ya hali mazingira nchini ya mwaka 2014 uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Aidha alisema hali hiyo inatokana na wananchi kutokupata elimu ya kutosha juu ya utunzaji wa mazingira pamoja na upungufu katika utekelezaji wa sheria, kanuni na mikakati ya utunzaji wa mazingira.
"Wananchi bado wanahitaji elimu ya kutosha kwani inaonekana uharibifu mkubwa wa mazingira unatokana na shughuli za kibinadamu zisizozingatia kanuni za utunzaji wa mazingira kama vile viwanda, kilimo, uvuvi, ufugaji na makazi. " alisema Dk Mahenge.
Pamoja na sheria ya mazingira ya mwaka 2004 kutaka ripoti ya mazingira itolewe kila baada ya miaka miwili, Dk. Mahenge alisema imekuwa vigumu kutekeleza sheria hiyo ikiwa ni miaka sita sasa tangu kutolewa kwa ripoti ya kwanza mwaka 2008 na kusema changamoto kubwa ni ufinyu wa bajeti na hivyo kuitaka serikali kubadilisha sheria ili muda wa kutoa ripoti uongezwe.
Akizungumza baada ya uzinduzi wa ripoti hiyo Mbunge wa Viti Maalumu na mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Mazingira, Ester Bulaya alisema hakubaliani na pendekezo la waziri kutaka muda wa kutoa ripoti upunguzwe.
"Ripoti inaonyesha uharibifu wa mazingira unaongezeka na hivyo lazima ripoti itolewe kwa wakati uliopangwa kisheria na suluhu ni kutafuta fedha za kutosha si kupunguza muda kwani kila kukicha mazingira yanaharibika," alisema Bulaya.
Mwisho