Tuesday, April 21, 2015

FUNDI MIAVULI AFIA NDANI KWAKE, AHARIBIKA!


FUNDI MIAVULI AFIA NDANI KWAKE, AHARIBIKA!

Wakazi wa Mtoni Kwa Aziz Ally, jijini Dar, wiki iliyopita walipatwa na mshangao baada ya mzee mmoja, Hamisi Mzee Hamisi kukutwa chumbani kwake akiwa amefariki dunia.Mzee huyo ambaye alikuwa ni fundi miavuli maeneo ya Kariakoo, inadaiwa hakuonekana nyumbani kwake kwa siku sita mfululizo huku mlango wake ukiwa wazi.
"Kilichotushitua majirani ni harufu kali iliyokuwa ikitokea eneo la usawa wa nyumba ya mzee huyo," kilisema chanzo.
 "Harufu ile ilianza kusikika muda mrefu na ilikuwa kali sana, baada ya kuifuatilia ndipo ikabainika ilitokea chumbani kwa mzee Hamisi, baada ya kuingia ndipo alikutwa akiwa amekufa huku mwili wake ukiwa umeharibika vibaya, wadudu wakiwa wameuzunguka na kutambaa chini,'' kilisema.
Kwa mujibu wa chanzo chetu, inasemekana marehemu alikuwa anaishi na kijana wake ambaye hakufahamika jina mara moja baada ya mkewe kuondoka miaka kadhaa iliyopita. Hata hivyo, kijana huyo inasemekana hajaonekana nyumbani hapo kwa siku sita.
Kwa mujibu wa chanzo chetu, mzee Hamisi hakuwa na ndugu yeyote anayefahamika eneo hilo.

Polisi wa Kituo cha Chang'ombe walifika nyumbani kwa mzee huyo baada ya kupewa taarifa na mmoja wa wananchi wa eneo hilo ambapo waliuchukua mwili wa marehemu na kuupeleka Hospitali ya Temeke kwa ajili ya kuufanyia uchunguzi zaidi.