Friday, March 13, 2015

BoT yasema haijui mabilioni ya Uswisi.



BoT yasema haijui mabilioni ya Uswisi.
Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Juma Reli.

Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Juma Reli, amejikaanga kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), akieleza kuwa benki hiyo haifahamu wala haijafuatilia taarifa za akaunti 99 zinazodaiwa kumilikiwa kinyemela na Watanzania kwenye akaunti za siri nchini Uswisi.

Aidha, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imesema imeanza kuchunguza taarifa zilizotolewa na ripoti ya mtandao wa Swiss Leaks chini ya Waandishi wa Habari za Uchunguzi wa Kimataifa (ICIJ) iliyowataja vigogo 99 wenye akaunti za siri nchini Uswisi ili kubaini majina yao kwa nia ya kuwatoza kodi. 

TRA imesema inakadiriwa kuwa takribani dola za Marekani milioni 328 (Sh. bilioni 574) zinapotea kutokana na utoroshwaji huo wa fedha.

Katika kikao hicho, majibu ya Naibu Gavana yalionyesha kuwakera wajumbe wa PAC ambao walimjia juu na kuhoji sababu za BoT kutofuatilia tuhuma hizo ilhali Serikali ya Uswiss ipo tayari kutoa ushirikiano.

Aliyeanza kumhoji Reli ni Mbunge wa Tabora Mjini, Ismail Aden Rage, ambaye alisema Septemba 24, 1998, BoT ilitoa waraka unaozuia Mtanzania kufungua akaunti nje ya nchi bila kibali.

Rage pia alihoji kama Watanzania wanafuata utaratibu huo na BoT imeshatoa vibali vingapi.

Akijibu, Reli alisema waraka huo bado upo lakini akasema watu binafsi hawaufuati kwa kuwa BoT haijawahi kupokea maombi ya watu binafsi kutaka vibali vya kufungua akaunti nje, licha ya kwamba wapo wanaomiliki akaunti kwa siri.

Alisema BoT imekuwa ikitoa vibali kwa kampuni za madini pekee, ambazo hata hivyo, taarifa za akaunti hizo haziwasilishwi TRA kwa ajili ya kukadiria kodi.

Majibu hayo yaliwakera wabunge na ndipo Mwenyekiti wa PAC,  Zitto Kabwe, alihoji kama kwa waraka huo, Watanzania wanaruhusiwa kufungua akaunti nje.

Swali hilo lilijibiwa na Katibu wa BoT ambaye pia ni Mwanasheria wa benki hiyo, Yusto Tongola, ambaye alisema kwa mujibu wa Sheria inayohusu ubadilishaji wa fedha za kigeni ya mwaka 1992, inatoa kibali kwa Mtanzania kufungua akaunti ya fedha za kigeni nchini, lakini siyo nje ya nchi.

Kufuatia majibu hayo, wabunge wa Viti Maalum (Chadema), Lucy Owenya na Zainabu Kawawa (CCM), walihoji kama BoT imefanyia kazi taarifa za Swissleaks.

Akijibu, Naibu Gavana Reli, alisema hawajachukua hatua zozote kuhusu vigogo 99 wa Tanzania wanaotuhumiwa kufungua akaunti za siri  Uswisi kwa kuwa hawana taarifa za kina.

Baada ya majibu hayo, Zitto alisema: " (jambo mahsusi) ya HSBC ninyi mmechukua hatua gani? Kuna taarifa kwamba maofisa wa hii benki walikuja nchini na kufanya mazungumzo na wateja wao wakati sheria inazuia, HSBC ina leseni ya kufanya biashara hapa nchini?"

Akijibu, Reli alisema sheria inaizuia benki isiyo na leseni kutafuta wateja nchini, lakini hawajapata taarifa hivyo hawajafuatilia.

"Hizo taarifa si za kwenye mitandao ya kijamii? Hatujazisoma na hatujazifanyia kazi. Labda tuzichukue sasa," alisema Reli.

Hata hivyo, Kamati ilishangazwa na majibu hayo na Zitto alimwambia kamati yake hairidhishwi na utendaji huo kwa kuwa jambo hilo ni zito.

Reli aliomba kupewa muda zaidi ili akazifanyie kazi na kuleta taarifa kwenye kamati.

Baada ya mahojiano hayo, PAC imeiagiza BoT kufanya utafiti wa kina kuhusu vigogo 99 wanaotajwa kuwa na akaunti za siri Uswisi na kuiwasilisha kwa kamati hiyo kabla ya Mei 15.

Aidha, PAC imemwagiza Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kuwasilisha taarifa ya kamati iliyokuwa inashughulikia mabilioni ya Uswiss kwenye Mkutano ujao wa Bunge.

Awali, Reli alisema BoT imeunda kikosi kazi cha wataalamu wa kimataifa kuchunguza kiasi cha fedha haramu kilichofichwa na Watanzania nje ya nchi, lakini hawatatafuta majina ya watu wala kampuni.