MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), imeshusha kidogo bei ya umeme kuanzia Machi Mosi mwaka huu, huku ikisisitiza kwamba bei hiyo itaendelea kupungua zaidi mradi wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam utakapoanza kazi.
Taarifa za hivi karibuni, zimeeleza kuwa bomba hilo limekamilika kwa asilimia 99 na kinachosubiriwa ni pamoja na majaribio ya usafirishaji wa gesi hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Felix Ngamlagosi, alisema kushuka kwa gharama hizo kunatokana na mabadiliko ya gharama za Shirika la Umeme (Tanesco), kutokana na mabadiliko katika bei ya mafuta, thamani ya fedha na mfumuko wa bei.
"Ukilinganisha makadirio yaliyofanywa na Ewura mwaka 2013, mahitaji ya pato la Tanesco kwa mwaka 2014 yanapunguzwa kwa kiasi cha Sh bilioni 33. Punguzo hili linashusha bei ya umeme ya wastani kutoka Sh 257.39 kwa uniti moja hadi Sh 251.70 kwa uniti moja sawa na asilimia 2.21," alisema.
Alisema kwa wateja wenye matumizi ya kawaida, bei ya umeme itashuka kutoka Sh 306 kwa uniti hadi Sh 298 kwa uniti sawa na punguzo la Sh nane.
Kwa bei hiyo ya watumiaji wa kawaida, umeme wa Sh 10,000 kwa bei ya zamani mtumiaji alikuwa akipata uniti 32.67, sasa kwa bei hiyo atapata uniti 33.5, ambayo ni ongezeko la uniti 0.88.
"Kwa wateja wenye matumizi ya kawaida kwa kupitia volti 400, bei ya umeme itashuka kutoka Sh 205 kwa uniti hadi Sh 200 kwa uniti sawa na punguzo la Sh tano kwa uniti," alisema.
Alisema kwa wateja waliounganishwa katika msongo wa kati wa umeme, bei ya umeme itashuka kutoka Sh 163 kwa uniti hadi Sh 159 kwa uniti sawa na punguzo la Sh nne kwa uniti moja.
Ngamlagosi alisema kwa wateja waliounganishwa katika msongo mkubwa wa umeme, vikiwemo viwanda, migodi na Zanzibar bei ya umeme itashuka kutoka Sh 159 kwa uniti hadi Sh 156 kwa uniti sawa na punguzo la Sh tatu kwa uniti.
"Kwa wateja wa majumbani wenye matumizi madogo ya wastani wa uniti 75 kwa mwezi, bei ya umeme haitabadilika kutokana na kwamba kundi hilo bei yake ni chini kutokana na gharama zake kuchangiwa na kundi la wateja wakubwa wa majumbani," alisema.
Ngamlagosi alisema Desemba 10 mwaka 2013 Bodi ya Wakurugenzi ya Ewura ilitoa agizo la mabadiliko ya bei ya umeme unaouzwa na Tanesco kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia 2014 hadi 2016 na zilianza kutumika mwaka jana.
Alisema kulingana na agizo hilo na kipengele cha saba cha kanuni za Kupanga Bei ya Umeme, bei za umeme zinatakiwa kurekebishwa kila baada ya miezi mitatu, kutokana na mabadiliko ya bei ya mafuta, thamani ya Shilingi ya Tanzania na mfumko wa bei na marekebisho hayo yanahusu bei ya kununua uniti ya umeme na si kwa tozo za mwezi.