Utafiti wa Sauti ya Wananchi ya Twaweza kwa kushirikiana na Taasisi ya Maendeleo ya Kimataifa (SID), kuhusu mustakabali wa nchi ifikapo 2025, umebaini mtu mmoja kati ya wanne kwenye kundi la matajiri, ana amini kuwa Tanzania itakuwa mahali pabaya pa kuishi ifikapo mwaka huo.
mujibu wa Mtafiti Mwandamizi wa taasisi hiyo, Edmund Matotay, utafiti huo wa awamu ya 23 ulifanyika kwa njia ya upigaji simu kati ya Agosti 13 hadi 22, mwaka jana na kujumuisha wahojiwa 1,408 ili kupata maoni yao juu ya mustakabali wa Tanzania.
Alisema wananchi wawili kati ya watatu wana amini kuwa nchi itakuwa mahali pazuri pa kuishi ifikapo mwaka huo, idadi ambayo inatofautiana kidogo tu kwa kulinganisha kati ya wananchi maskini zaidi na matajiri.
Alisema maskini wana matumaini zaidi kwa asilimia 68, wakati matumaini ya matajiri ni asilimia 64.
Hata hivyo, alisema tofauti hizo hazina maana kubwa kitakwimu, kwani zinaonyesha kuwa mtu mmoja kati ya wanne kwenye kundi la wananchi matajiri anaamini nchi itakuwa mahali pabaya pa kuishi ifikapo mwaka huo.
Aliyataja mambo mengine katika utafiti wao kuwa wananchi tisa kati ya 10 wana amini kwamba maamuzi muhimu yatabaki chini ya udhibiti wa kitaifa.
"Kama wanavyo amini kuwa hatma ya ustawi wa maisha ya baadaye iko mikononi mwao wenyewe, wananchi tisa kati ya 10 wana amini pia kuwa mustakabali wa Tanzania uko mikononi mwa Watanzania wenyewe, ama kwa kupitia viongozi wa nchi au wananchi wenyewe," alisema.
Alisema wawekezaji wa kigeni na wafadhili wanaonekana kuwa na udhibiti kidogo sana kwenye masuala muhimu.
"Mfano, hakuna mtu hata mmoja aliyetaja Umoja wa Mataifa kuwa na udhibiti" alisema.
Alisema kutokana na nchi kutegemea misaada ya wafadhili katika kuchangia bajeti na kutokana na uwekezaji wa kigeni wa moja kwa moja kuchangia mapato kutokana na utalii na mauzo ya nje ya madini, haya ni matokeo ya kuvutia.
Alisema Watanzania wasomi wanaonekana kutokuwa na umuhimu mkubwa kwa asilimia 0.1 kati ya mtu mmoja ya watu 1,000 waliohojiwa.
Kuhusu utoaji huduma, ukuaji wa uchumi na umoja wa kitaifa, alisema ni vipaumbele vikubwa kwa siku zijazo.
Alisema wakati wananchi wanajibu swali lililouliza ni mambo gani wanafikiri yawe vipaumbele muhimu vya nchi kwa siku zijazo, mambo muhimu zaidi kwao yalikuwa ubora wa huduma za umma kama elimu na afya kwa asilimia 28.
Alitaja kibaumbele cha pili muhimu ni ukuaji wa uchumi asilimia 16, kulinda utambulisho wa taifa asilimia 11 na kulinda maliasili za taifa asilimia 11.
Kwa upande wa kukua kwa uchumi wa taifa, alisema utafiti umeonyesha wananchi saba kati ya 10 wana amini kuwa Tanzania itakuwa nchi yenye uchumi wa kati ifikapo mwaka huo.
Kuhusu masuala binafsi, alisema utafiti huo ulibaini kwamba mwananchi mmoja moja kati ya wawili anatarajia kwamba maisha yake yatakuwa bora zaidi siku zijazo.
Pamoja na hayo alisema, karibu wananchi saba kati ya 10 yaani asilimia 68 wanatarajia kuona Rais mwanamke katika kipindi cha miaka 10 ijayo.
CHANZO: NIPASHE