Friday, January 23, 2015

Ukawa wabuni mbinu mpya ya urais 2015



Ukawa wabuni mbinu mpya ya urais 2015 VIONGOZI UKAWA


KIKAO cha pamoja kilichowakutanisha viongozi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kimetoa mikakati ya pamoja ikiwamo kuandaa ratiba ya uteuzi wa wagombea wa nafasi ya urais kwa kila chama.

Hatua hiyo imekuja baada ya kikao cha siri cha siku mbili kilichowakutanisha viongozi wa juu wa Ukawa ambao ni Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, Freeman Mbowe (Chadema), James Mbatia (NCCR-Mageuzi) na Dk. Emmanuel Makaidi (NLD).
Chanzo cha kuaminika kilisema jana kuwa katika kikao hicho, viongozi hao wamekubaliana kuweka mikakati hiyo ikiwamo ya kushika dola katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba, mwaka huu.

Katika kikao hicho, viongozi hao wametoa ratiba ambayo inakitaka kila chama kuteua mgombea wake wa urais ili ajulikane mapema kabla vikao vya Ukawa kuteua jina la mgombea mmoja.


"Imewekwa mikakati hii kwa lengo la kuimarisha demokrasia kwa kila chama husika, hasa vinavyounda Ukawa vipate muda wa kutosha wa kuweza kufanya uteuzi mapema.


"Lakini pia sasa ni wakati kwa wale wazalendo wa kweli, hasa kutoka upande wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambao wana uchungu na nchi yao wajitoe mapema na kuja kushiriki uchaguzi kupitia Ukawa badala ya kusubiri hadi mwisho, kwani wakifanya hivyo wanaweza wakakuta milango imefungwa.


"Hili linaweza kuwafanya washindwe kupata nafasi sasa, maana ni wazi Ukawa ndiyo tegemeo la Watanzania wengi kwa sasa ambao wapo tayari kukabidhi dola katika uchaguzi ujao," kilisema chanzo hicho.


Mbali na kuweka mkakati hiyo, viongozi hao wa Ukawa wameandaa kanuni za uchaguzi ambazo kila chama kinatakiwa kuwasilisha katika vikao vyake vya uamuzi na kuweza kujadili kama njia ya kushika dola.


Mikakati hiyo ya Ukawa inatarajiwa kuwekwa wazi leo ambapo wenyeviti wote wanatarajiwa kuzungumza na waandishi wa habari.


Katika kinachoelezwa kutekeleza mikakati ya Ukawa, tayari Kamati Kuu ya Chadema, imekutana jijini Dar es Salaam ambapo ilijadili hali ya kisiasa nchini, Katiba inayopendekezwa na kanuni za uchaguzi za Ukawa kama njia ya kuelekea kuteua mgombea mmoja wa urais katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.


Pamoja na kuratibiwa kwa vikao vya Ukawa vya kupata mgombea mmoja wa urais, kwa upande wa CUF, wamekuwa wakipigana kufa na kupona kuhakikisha, Profesa Lipumba anakuwa mgombea wa urais kupitia umoja huo.


Nao Chadema wamekuwa wakiendesha harakati za kile kinachoelezwa kuhitajiwa na Watanzania kwa Dk. Willibrod Slaa kuwa mgombea urais kwa kigezo kwamba ana mvuto na kipenzi cha watu wengi hali iliyomfanya ashike nafasi ya pili katika Uchaguzi Mkuu uliopita.


Hata hivyo, katika harakati hizo tayari Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, Mbatia amekuwa katika harakati za kugombea ubunge katika Jimbo la Vunjo, huku Dk. Makaidi naye akitarajiwa kufanya hivyo.


Ikiwa Mbatia na Dk. Makaidi wataendelea na misimamo yao ya kuwania ubunge kinyang'anyiro cha kuwania urais kupitia Ukawa kitakuwa kwa Profesa Lipumba na Dk. Slaa.


Ushirikiano wa vyama hivyo ulianza katika Bunge Maalumu la Katiba na kuendelea hadi Bunge la Jamhuri ambapo vyama washirika viliingizwa kwenye baraza kivuli ambalo lilikuwa likiongozwa na Chadema peke yake.


Vyama hivyo vimepata msisimko zaidi katika umoja wao baada ya kufanikiwa kushinda viti vingi katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.