Waziri Mkuu Mizengo Pinda amesema kama Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) itaona muda wa uandikishaji wananchi katika Daftari la Wapigakura kwa ajili ya Kura ya Maoni ya Katiba Inayopendekezwa hautoshi, atawasilisha suala hilo bungeni ili uongezwe.
Pinda alisema hayo bungeni mjini Dodoma jana katika kipindi cha maswali kwa Waziri Mkuu bungeni alipokuwa akijibu swali la Kiongozi wa Kambi ya Upinzani, Freeman Mbowe aliyemtaka kueleza Serikali ina mpango gani kuhakikisha hakuna tatizo litakalotokea katika uandikishaji, hasa ikizingatiwa kuwa muda uliopo hautoshi na majaribio ya uandikishaji kwa BVR umeibua kasoro nyingi.
Akijibu swali hilo, Pinda alisema: "Aliyoyasema Mbowe, Serikali haiwezi kuyapuuza hata kidogo na ni kweli mchakato huo umekuwa na matatizo kidogo hasa ya fedha na Serikali imekuwa ikipambana ili kuweza kufanikisha mchakato huo," alisema Pinda.
Januari 20, Mwenyekiti wa Nec, Jaji Damian Lubuva alikaririwa akisema tume yake haijapata fedha kutoka serikalini, lakini kesho yake, mkurugenzi wa uchaguzi wa Nec, Julius Malaba alisema fedha zipo na mchakato wa uandikishaji na upigaji kura utakwenda kama ulivyopangwa, akisema utaanza Februari 16 na utamalizika kwa wakati.
Jana, Mbowe alisema majaribio ya uandikishaji wa kutumia mashine za kielektroniki za BVR katika majimbo ya Kawe, Wilaya ya Mlele na Kilombero yameibuka na changamoto mbalimbali na huku nchi ikitakiwa kuandikisha wapigakura zaidi ya milioni 24 na kuhoji kuhusu muda uliopangwa wa uandikishaji, hasa ikizingatiwa kuwa zimebaki siku 90 kufikia kwenye kura ya maoni huku mashine moja ikiwa na uwezo wa kuandikisha watu 22 kwa siku.
Akizungumzia suala hilo, Waziri Mkuu alisema BVR 250 zilizoingia kwa ajili ya majaribio zilikuwa ni za kupima uwezo wake na kukiri kwamba matatizo ya hapa na pale yalijitokeza na kuongeza kuwa yanashughulikiwa ili yasiwepo wakati kazi rasmi litakapoanza.
Alisema kwa taarifa alizopewa na Nec ni kwamba mashine moja ya BVR inaandikisha watu 70 kwa siku moja na siyo 22.
Mbunge wa Mkanyageni (CUF), Mohammed Habib Mnyaa alimtaka Waziri Mkuu kutoa ufafanuzi kuhusu mkanganyiko wa matumizi ya Vitambulisho vya Taifa ambavyo Rais alisema vingetumika kwenye Uchaguzi Mkuu, huku akisema kama Serikali haina fedha kwa nini mradi wa BVR na ule wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) usiwe mmoja ili vitambulisho vya Taifa vitumike kama Rais alivyosema.
Akijibu swali hilo, Waziri Mkuu alisema kumekuwa na mjadala mkubwa kuhusu hilo la mradi wa Nida na Nec kwa kuwa mamlaka hiyo ya vitambulisho ndiyo iliyoanza na Nec ikafuatia.
Pinda alisema Nida iliahidi kuwa ingemaliza uandikishaji kabla ya Uchaguzi Mkuu lakini Nec haina muda maalumu hivyo Nec itaendelea ili kukamilisha ndani ya muda iliojipangia.