Friday, January 23, 2015

Makongoro Nyerere achaguliwa kuwa mwenyekiti bunge la afrika mashariki amrithi Kimbisa



Makongoro Nyerere achaguliwa kuwa mwenyekiti bunge la afrika mashariki amrithi Kimbisa


Wabunge wa Tanzania kwenye Bunge la Afrika ya Mashariki (Eala) wamemchagua Makongoro Nyerere kuwa mwenyekiti wao mpya baada ya Adam Kimbisa kumaliza muda wake.

Uchaguzi huo uliofanyika juzi, Twaha Taslima alichaguliwa kuwa katibu, nafasi iliyokuwa ikishikiliwa na Shyrose Bhanji.

Viongozi hao wapya watashikilia nyadhifa hizo kwa kipindi cha miaka miwili na nusu. Uchaguzi kama huo pia umefanyika katika nchi za Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi. Kimbisa na Shy-Rose walikuwa makamishna kuanzia Juni 5, 2012 hadi Desemba 2014.

Wakati huohuo, wabunge wa Tanzania wamefafanua habari kuwa hawakuhudhuria mkutano wa waandishi wa habari na Spika mpya wa Bunge hilo juzi, Dan Kidega. Mwenyekiti huyo mpya wa Eala, Nyerere alisema siyo kweli kwamba wabunge saba wa Tanzania hawakuhudhuria kikao cha Bunge hilo lililoanza Jumatatu, bali usahihi ni kwamba wabunge wanane kati ya tisa kutoka Tanzania walihudhuria na siyo watatu tu.

kama ilivyoripotiwa.

Alisema wabunge wanane waliohudhuria kikao hicho ni pamoja na Adam Kimbisa, Shy-Rose Bhanji, Bernard Murunya, Abdullah Mwinyi, Angella Kiziga, Nderakindo Kessy na Maryam Ussi wakati ambaye hakuhudhuria ni Twaha Taslima.

Hivi karibuni Bunge hilo limejikuta likiandamwa na migomo na vurugu za hapa na pale na kusababisha kuahirishwa mara kwa mara.

Aliyekuwa Spika wa Bunge hilo, Margaret Zziwa alivuliwa madaraka Desemba, mwaka jana baada ya wabunge kupiga kura ya kumkataa.

Kuondolewa kwa Zziwa kulitokana na wabunge hao kuchoshwa na utendaji kazi wake. Idadi ya wabunge waliokuwapo ndani ya Bunge hilo ilikuwa ni 39.