Mabomu yaliyofatuliwa na Jeshi la Polisi Jumanne wiki hii kuwazuia wanachama na viongozi wa Chama cha Wananchi (CUF), wasifanywe maandamano yaliwaathiri watoto wa shule ya awali ya Mango (Madrasat Munawara), iliyopo Mtoni Mtongani, Temeke, Dar es Salaam.
Mwalimu wa shule hiyo, Nasra Mohamed, alisema hakuna mtoto aliyepotea kutokana na tukio la mabomu, lakini moshi wa mabomu uliwachanganya na kukimbia ovyo.
Alisema watoto wote walikimbilia nyumbani kwao, lakini walipoteza vitu mbalimbali walipokuwa wakikimbia ili kunusuru maisha yao kutokana na mabomu yakiyokuwa yakipigwa mfululizo.
"Mimi mwenye nilikuwa nalia kama mtoto mdogo ili kuwanusuru wanafunzi wangu, nilinawa maji ya kuoshea chipsi, lakini kama nisingepata maji hayo hali ilikuwa mbaya sana kwangu," alisema.
Nasra alisema wakati mabomu hayo yanapigwa alikuwa kwenye kibanda cha chipsi, hivyo alimwona askari mmoja akiwa kwenye makutano ya barabara ya Mtongani akipiga mabomu mfululizo, kitendo kilichofanya akimbie haraka hadi shuleni kuwahi wanafunzi.
Alisema alipofika alikuta watoto wote wanakohoa na kutupa viti vyao mbalimbali na kukimbia hovyo.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Mtongani, Khamis Mtonga, alisema Serikali haikupaswa kutumia nguvu kubwa katika kuzuia maandamano bali hekima na busara ilipaswa kuzingatiwa kuhakikisha usalama wa raia unaimarishwa kwenye mkutano huo.
Mtonga alisema kuwa taharuki hiyo ilisababisha baadhi ya watu wasio na hatia, wakiwamo watoto kukimbia hovyo kwa nia ya kuokoa usalama wao.
"Bado sijapata taarifa ya mtoto au mtu mzima aliyepata madhara kutokana na milipuko ya mabomu hayo bali ilikuwa patashika mtaani," alisema.
Wanachama, wapenzi na viongozi wa CUF akiwamo Mwenyekiti wake wa Taifa, Profesa Ibrahim Lipumba walipigwa mabomu na kukamatwa na polisi wakidaiwa kutaka kuandamana bila kibali.
Wanachama hao walikuwa wameandaa maandamano kutoka ofisi za CUF Wilaya ya Temeke hadi viwanja vya Zamkhen, Mbagala kwa ajili ya mkutano wa hadhara.
Lengo na maandamano na mkutano huo lilikuwa ni kumbukumbu ya miaka 14 ya wenzao zaidi ya 30 waliouawa na Jeshi la Polisi mwaka 2001 wakati wakipinga matokeo ya uchaguzi mkuu wa Rais wa Zanzibar wa mwaka 200.
CHANZO: NIPASHE