Wazazi nchini Tanzania wametakiwa kuzungumza na watoto wao umuhimu wa elimu na hali halisi ya maisha ili kuepuka kujiingiza kwenye vitendo viovu ikiwamo mimba za utotoni na maambukizi ya ukimwi.
Hayo yamesema na Mkurugenzi wa Chama cha Uzazi na Malezi Bora Tanzania (UMATI) Lulu Ng'wanakilala katika maadhimisho ya kupinga unyanyasajji kwa watoto pamoja na maambukizi ya ukimwi nchini.
"Wazazi na jamii kwa ujumla wanapaswa kukemea tabia ya unyanyasaji hasa wanafunzi wanaofanyiwa na makondakta wa dala dala, wanapowasukuma kuwazuia kupanda na huku wengine wakitumia fursa hiyo ya shida ya usafiri kuwahadaa watoto wa kike kwa kuwataka kimapenzi.
"Kuna wanaume watu wazima lakini wana kazi ya kuwatongoza watoto wadogo kwa kuwahada na pesa, zawadi kwa lengo la kuwashawishi na kujaamia nayo, makonda wa dala dala nao ndio usiseme, jamii inapaswa kukemea kwa nguvu zote jambo hili, kwa kuwachukulia hatua bila hivyo vitendo hivyo viovu haviwezi kuisha.
"Watu wazima wanashuhudia wanafunzi wanavyosukumwa na makondakta na kuambiwa wasipande dala dala, wao wanapanda wanawaacha wanafunzi chini, si haki kabisa, kupitia mradi huu wa jamvi la vijana tunapiga vita unyanyasaji wa vijana kwa nguvu zote." alisema Ng'wanakilala.
Alisema pia kupitia mradi huo wa Jamvi la Vijana, wamekuwa wakitoa elimu kwa vijana ikiwemo kupima kwa hiyari maambukizi ya VVU, saratani ya shingo ya kizazi kwa kuwa moja ya sababu ya ugojwa huo ni kujiingiza kwenye vitendo vya ngono zisizo salama katika umri mdogo.
"Tanzania hii kuna maeneo mtoto wa miaka tisa ana mtoto, wazazi wanawafukuza nyumbani huu ni ukatili wa hali ya juu, ukatili kwa kupewa mimba akiwa na umri mdogo, na ukatili kwa kufukuzwa nyumbani ndio chanzo kikuu cha watoto wa mitaani na wengine kuamua kuwatupa na hata kuwaua, ndio maana tumeamua tutoe elimu hii kwa vijana.
Alisema kupitia mradi huo wa Jamvi la Vijana ambao wanazunguka sehemu mbalimbali lengo lao ni kuwafikia vijana 200 kila mwezi na vijana 1,000 kwa mwaka.
Mkurugenzi wa Chama cha Uzazi na Malezi Bora Tanzania (UMATI), Lulu Ng'wanakilala (kushoto) akizungumza katika tamasha la Jamvi la Vijana lililofanyika kwenye ofisi za Umati Temeke,jijini Dar es Salaam. kulia ni ofisa habari wa Umati, Upendo Daud.
Sehemu ya vijana waliojitokeza kwenye tamasha hilo
Sehemu ya washiriki kwenye igizo linalopinga unyanyasaji kwa vijana.