Wednesday, December 31, 2014

MTIBWA FC WAAHIDI UTAMU KOMBE LA MAPINDUZI


MTIBWA FC WAAHIDI UTAMU KOMBE LA MAPINDUZI

mtibwa v yanga

Na Bertha Lumala, Dar es Salaam
Vinara wa msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), Mtibwa Sugar FC wamewaahidi wapenzi wa soka visiwani Zanzibar kufurahia makali yao ya msimu huu watakaposhiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi mwakani.

Mtibwa Sugar FC, mabingwa wa Tanzania Bara 1999 na 2000, ni miongoni mwa timu nne za VPL zilizoalikwa na Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) kushiriki michuano hiyo itakayoanza Januari 1-13 mwakani.

Msemaji wa Mtibwa Sugar FC, Thobias Kifaru, amesema kikosi chao bado kiko Manungu, Turiani, km 100 kutoka mjini Morogoro na muda wowote kuanzia Jumatano asubuhi kitaanza safari kuelekea Zenj.

"Tumefanya vizuri katika Ligi Kuu ya Vodacom. Wazanzibar watarajie utamu kutoka kwetu. Tunahamishia makali yetu ya Bara huko Zanzibar," amesema Kifaru.

Mbali na timu nne zaa Tanzania Bara. Mtibwa, AzamFC, Yanga SC na Simba SC, timu nyingine nane zimealikwa kushiriki michuano hiyo inayofanyika kwa mara ya tisa tangu ianzishwe kuenzi Mapinduzi Tukufu ya Zanzibar yaliyofanyika Januari 12, 1964.

Timu hizo ni pamoja na mabingwa watetezi KCC FC ya Uganda, mabingwa wa Zanzibar KMKM, Mafunzo FC, Shaba FC ya Pemba, Police Zanzibar, Mtende Rangers, JKU FC na Ulinzi FC ya Kenya huku mabingwa mara 19 wa Ligi Kuu ya Sudan, El Merrikh wakiomba pia kushiriki.