MTANZANIA anayetumikia kifungo cha miaka 30 jela baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la unyang'anyi wa kutumia silaha, Alex Thomas amepeleka hukumu yake mbele ya Mahakama ya Afrika (AfCHPR) akidai kwamba haki zake za msingi zimekiukwa.
Madai hayo yatasikilizwa Desemba leo na mahakama hiyo inayoketi katika kikao chake cha kawaida mjini Addis Ababa, Ethiopia, linaripoti Shirika Huru la Habari la Afrika Mashariki (EANA).
Mwaka 1998 Mahakama iliyokuwa inasikiliza kesi yake nchini Tanzania ilimtia hatiani Thomas kwa kosa la unyang'anyi wa kutumia silaha na kuhukumiwa kifungo cha miaka 30.
Anatumikia adhabu hiyo katika Gereza Kuu la Karanga mkoani Kilimanjaro ambapo mwaka 2009 Mahakama ya Rufaa ya Tanzania ilithibitisha hukumu hiyo baada ya rufaa yake kutupwa.
Juhudi zake za kutaka kesi yake isikilizwe upya zinadaiwa kukwama kwa sababu hakuna hatua zozote zilizofanyika kuhusu ombi hilo.
Juni 2009, Thomas aliwasilisha maombi yake Mahakama ya Afrika akitaka mahakama hiyo ipitie upya hukumu ya Mahakama Kuu ya Tanzania, kwa madai kwamba mfumo wa haki katika mahakama za Tanzania unachelewesha kwa makusudi kutoa uamuzi wa maombi yake ya kutaka kupitiwa upya kwa hukumu dhidi yake.
Katika maombi hayo Thomas anadai kwamba usikilizwaji wa kesi yake mbele ya mahakama za Tanzania kulikabiliwa na mapungufu mengi.
Anadai miongoni mwa mapungufu hayo ni pamoja na mahakama kukosa mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo kwa kuwa unyang'anyi uliodaiwa kufanywa ulifanyika nchini Kenya.
Pia anadai kwamba mwendesha mashitaka hakuthibitisha pasipo mashaka mashitaka dhidi yake kwa kuwa ushahidi alioutoa unatia shaka hususan suala la Thomas kutumia bunduki katika kutenda kosa hilo na umiliki wa silaha yenyewe ambayo pia ilidaiwa kuwa aliiba.
Pamoja na madai hayo, Thomas pia anadai kwamba amenyimwa haki ya kusikilizwa na kwamba hakupatiwa wakili wa kumtetea kama Katiba ya Tanzania inavyotaka.
Thomas anaiomba Mahakama ya Afrika kutengua hukumu iliyotolewa na Mahakama ya awali na hukumu iliyothibitisha adhabu dhidi yake iliyotolewa na Mahakama Kuu ya Tanzania ikiwa ni pamoja na kumwona hana hatia na kisha kumwachia huru.
HABARI LEO