Friday, December 05, 2014

ICC yatupilia mbali kesi ya Kenyatta


ICC yatupilia mbali kesi ya Kenyatta
Mahakama ya kimataifa ya ICC imetupilia mbali kesi ya jinai inayomkabili Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta.

Mwendesha Mashtaka mkuu, Fatou Bensouda ameondoa kesi dhidi ya Kenyatta ambaye alidaiwa kutenda uhalifu dhidi ya binadamu wakati wa ghasia za baada ya uchaguzi wa mwaka 2007/2008 nchini humo.

Mahakama ilikuwa imempa Bensouda wiki moja kuamua ikiwa ataendelea na kesi dhidi ya Kenyatta au la ingawa alisema muda huo haukutosha kwake yeye kuandaa ushahidi zaidi dhidi ya Kenyatta.

Kenyatta alishtakiwa kama mshukiwa mkuu wa ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007/2008 akituhimiwa pamoja na William Ruto ambaye ni Naibu Rais wa nchi hiyo ya Kenya kwa kutenda uhalifu dhidi ya binadamu.

Zaidi ya watu elfu moja waliuawa wakati wa ghasia hizo. 

Uhuru alikuwa mtu maarufu zaidi kufikishwa mahakamani na pia mshukiwa mkuu kwani alifikishwa mahakamani akiwa Rais aliye mamlakani.

Hili ni pigo kubwa kwa upande wa mashitaka, wengi walioana kesi dhidi ya Kenyatta kama mtihani mkubwa katika historia ya mahakama hiyo.

Upande wa mashitaka ulitaka mahakama kuupatia muda zaidi ili upate ushahidi zaidi,dhidi ya Kenyatta kama vile taarifa za akaunti yake ya benki.
Upande wa utetezi ulisema kuwa ikiwa hakuna ushahidi wa kutosha kesi hiyo inapaswa kutupiliwa mbali.

CHANZO: BBC SWAHILI