Mkurugenzi wa Serikali za Mitaa bwana Kharist Michael Luanda akitangaza idadi ya watanzania waliojiandikisha kushiriki uchaguzi wa serikali za Mitaa utakaofanyika jumapili ijayo.
Jumla ya Watanzania 11,491,661 sawa na asilimia 62% ya watanzania 18,587,742 ambao walitarajiwa kujiandikisha kushiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika jumapili ijayo wamejiandikisha kushiriki uchaguzi huo. Mkurugenzi wa Serikali za Mitaa katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali Mitaa Bwana Kharist Michael Luanda aliwaambia waandishi wa habari mjini Dodoma kuwa mikoa ambayo imeandikisha idadi kubwa ya wapiga kura ni Katavi 79% na Kagera (78%) na mikoa ambayo iliandikisha idadi ndogo ya wapiga kura ni Dar es salaam 43% na Kilimanjaro 50% .
Aidha alizitaja Halmashauri ambazo zimeandikisha idadi kubwa ya wapigakura kuwa ni Halmashauri ya mji wa Mpanda 107% na Halmashauri mji wa Babati 101%. Halmashauri ambazo hazikufikia hata nusu ni Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi 21% na Halmashauri ya Wilaya ya Same 22%.
Alisema kila Halmashauri imeandaa karatasi za kupigia kura ambazo zitakuwa na Jina la mgombea, Jina la Chama, Nembo ya chama na nembo ya Halmashauri,hivyo kila mpiga kura atatakiwa kuweka alama ya vyema katika kisanduku kilicho chini ya Nembo ya chama kuonyesha kuwa amempigia kura mgombea aliyetaka kumchagua.
Bwana Luanda alisema kuwa vituo vya kupiga kura vitakuwa katika majengo ya Umma isipo kuwa katika vituo vya Polisi, kanisani au msikitini na katika vituo vya Afya. Aliongeza kuwa pale ambapo hakuna majengo ya Umma Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi atashauriana na Vyama vya Siasa kuandaa sehemu maalum ya kupigia kura.
Bwana Luanda alisema vituo vitafunguliwa kuanzia saa 2:00 asubuhi mpaka saa 10:00 jioni, wapiga kura watakaokuwepo kituoni saa 10:00 jioni wataruhusiwa kupiga kura hadi watakapokuwa wamemaliza kupiga kura.
Mkurugenzi huyo aliongeza kuwa wakati wa kupiga kura kabla Msimamizi Msaidizi wa uchaguzi hajampa karatasi za kupiga kura atajiridhisha kama jina la mpiga kura limeorodheshwa katika Orodha ya wapiga kura na baada ya kuridhika atamtaka ajitambulishe kwa kutumia kitambulisho kimoja kati ya Kitambulisho cha Mpiga kura cha Uchaguzi Mkuu, kazi, Hati ya kusafiria, Kadi ya Benki, Kadi ya Bima ya Afya, Shule au Chuo, Leseni ya Udereva na kitambulisho cha Uraia.
"Ikiwa Mpiga Kura atakuwa hana kitambulisho cha aina yoyote kichotajwa katika kanuni za Uchaguzi lakini jina lake limo kwenye orodha ya Wapiga Kura, Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi atamruhusu mtu huyo kupiga kura baada ya kutambuliwa na wakazi wa eneo husika" alisema.
Bwana Luanda ametoa rai kwa watanzania wote waliojiandikisha kupiga kura wajitokeze kwa wingi siku ya juma pili kwenda kupiga kura. Pia ameviomba Vyama vya Siasa na viongozi wa Asasi zisizo za Kiserikali kuhamasisha wapiga kura kujitokeza kwa wingi kuchagua Viongozi wao.
Aidha Mkurugenzi huyo wa TAMISEMI aliwaonya wananchi kutopiga kura zaidi ya mara moja au kutaka kupiga kura endapo hawakujiandikisha kushiriki uchaguzi huo kwani ni kosa la jinai na hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya yeyote atakaye jaribu kukiuka Sheria, Kanuni na Taratibu za Uchaguzi.