Tuesday, November 18, 2014

Vijana waaswa kushiriki mashindano ya teknolojia



Vijana waaswa kushiriki mashindano ya teknolojia
Meneja Uhusiano wa Nje wa Vodacom Tanzania,Abigail Ambweni akiwafafanulia jambo baadhi ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kutoka Kitivo cha Sayansi ya Kompyuta kuhusiana na shindano la AppStar linaloendeshwa na kampuni hiyo linalowalenga wataalam wa kutengeneza mobile applications na kujishindia zawadi mbalimbali ikiwemo pesa taslim na safari ya kwenda nchini India kushiriki katika shindano hilo ngazi ya kimataifa.
Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wa Kitivo cha Sayansi ya Kompyuta,John Marolera akimuulizawa swali Meneja Uhusiano wa Nje wa Vodacom Tanzania,Abigail Ambweni kuhusiana na shindano la AppStar linaloendeshwa na Vodacom Tanzania linalowalenga wataalam wa kutengeneza mobile applications na kujishindia zawadi mbalimbali ikiwemo pesa taslim na safari ya kwenda nchini India kushiriki katika shindano hilo ngazi ya kimataifa.
Baadhi ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wa Kitivo cha Sayansi ya Kompyuta,wakielekea katika sehemu maalum ya kupatiwa maelezo ya jinsi ya kushiriki katika shindano la AppStar linaloendeshwa na Vodacom Tanzania linalohusiana na wataalam wa kutengeneza mobile applications kushiriki katika shindano hilo na kujishindia zawadi mbalimbali ikiwemo pesa taslim na safari ya kwenda nchini India kushiriki katika shindano hilo ngazi ya kimataifa.

Ndoto za wanafunzi wa vyuo vikuu wanaosoma masomo ya sayansi ya teknokojia ya habari na mawasiliano nchini ya  kuwa magwiji wa fani hiyo zinaelekea kutimia. Hali hii inatokana na  kuzinduliwa kwa shindano la kusaka vipaji vya ugunduzi wa program za simu  - App Star – mwezi huu.

Shindano hili la kimataifa lilizinduliwa na Kampuni ya mawasiliano ya Vodacom Tanzania na linajumuisha Watanzania wote wenye hamasa ya kutumia teknolojia kuboresha maisha yao na ya jamii zao kwa ujumla.  Aidha, ngwe ya kwanza ya kuchuja majina ya wale watakaoshiriki  katika  duru ya mwisho ya mashindano hayo itakayofanyika mjini Bangalore, nchini India itafanyika tarehe 5 Disemba 2014 jijini Dar es Salaam.

Kwa upande wake Meneja wa Mahusiano ya Nje wa Vodacom Tanzania, Abigail Ambweni ambaye aliyekuwa katika harakati za kuwahamasisha wanafunzi wanaosoma masomo ya kompyuta katika Kitivo Cha Sayansi ya Kompyuta cha Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, aliwasihi vijana hao  kushiriki katika shindano hilo ambalo pamoja na mambo pengine pia linalenga kuibua vipaji vya vijana kwenye nyanja ya  ubunifu wa teknolojia.

"Dunia ya sasa ni ya sayansi na teknolojia hivyo tunaamini kuwa ubunifu wa programu za kiteknolojia haunufaishi mbunifu peke yake bali pia hurahisisha maisha ya wananchi wote wanaoitumia program hiyo. Hivyo basi, huu ni wakati wenu vijana kujitokeza  na kuvinadi vipaji vyenu kupitia shindano hili", alisema Ambweni.

Baadhi ya wanafunzi wa Chuo hicho walihamasika kushiriki na wameipongeza Vodacom kwa kuandaa shindano kama hili lenye mwelekeo wa kuinua vipaji na wametoa ushauri kuwa shindano hilo lisiishie kwenye ubunifu wa programu za simu bali ubunifu wa kila aina wa matumizi ya kompyuta.

Ambweni aliendelea kusema kwamba Shindano hili liko wazi kwa wabunifu  na watumiaji wote wa teknolojia wanaotumia mifumo mbalimbali kama vile  Android, Windows, IOS, Sumbian na nyinginezo na wanapaswa kuwasilisha kazi zao kabla ya tarehe ya mwisho ya kujisajili ya Novemba 25, 2014. Mshindi wa kwanza mwaka huu atazawadiwa pesa taslimu na atagharamiwa safari ya kwenda India kushiriki kwenye ngazi ya kimataifa ya shindano hili ambapo atakayeibuka mshindi huko atapata fursa ya kuhudhuria mkutano mkuu wa kimataifa  wa masuala ya simu za mkononi utakaofanyika Barcelona nchini Hispania.

Wabunifu wanaotaka kushiriki wametengwa katika makundi mawili mojawapo likiwa ni lile la wenye makampuni na tayari wana mitandao na wale ambao ndio kwanza kabisa wanawiwa kutangaza ubunifu wao. Washiriki wana uhuru wa kuchagua kushiriki katika kundi lolote wanalodhani linakidhi mahitaji yao.

Naye Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Intaneti wa Vodacom Tanzania Saurabh Jaiswal alisema, washiriki  wa shindalo hili mwaka jana walijikita katika ubunifu kwenye nyanja za michezo ya kwenye simu, elimu, burudani, michezo, afya, kilimo na mazingira.

"Tunawahimiza washiriki kutumia fursa hii kutangaza vipaji vyao na kuonyesha ubunifu wao wa kidijitali tulinao nchini Tanzania, " alisema Jaiswal.

Tangu kuanzishwa kwa mashindano haya mwaka 2012, washiriki wengi wenye vipaji vya ubunifu wa teknolojia wamendelea kuingia katika mchuano huu wa kiteknolojia. Wabunifu kutoka nchi za  Tanzania, Afrika ya Kusini, Misri, Kenya, Ghana na  India watashiriki katika mashindano ya mwaka huu. Maelezo zaidi ya shindano hili la App Star yanapatika dev.info@vodafone.com