Na Beatrice Lyimo- Maelezo.
GESI asilia ni bidhaa muhimu kwa maendeleo ya wananchi na uchumi wa nchi yeyote ikiwemo Tanzania.
Hayo yamesemwa leo na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Said Meck Sadick wakati wa ufunguzi wa taftishi juu ya maombi la Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kuhusu mapendekezo ya tozo ya uchakataji na usafirishaji wa Gesi asilia uliofanyika.
Mhe. Sadick amesema kuwa, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) ilipokea maombi ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kuhusu mapendekezo ya tozo ya uchakataji na usafirishaji wa Gesi asilia, hivyo EWURA inatarajia kuandaa mkutano wa wadau wa gesi asilia ili kupata maoni juu ya maombi hayo.
Alibainisha kuwa, kutokana na upungufu wa maji ya kuendeshea mitambo ya umeme uliosababishwa na ukame nchini Tanzania, zaidi ya asilimia 40 ya uzalishaji wa umeme kwa sasa unategemea hiyo.
“Gesi asilia inayozalishwa kwa sasa inategemewa katika uzalishaji wa umeme nchini ambapo asilimia 88 ya gesi hii inatumika katika kuzalisha nishati ya umeme”, alisema Mhe Sadick.
Aliongeza kuwa, mitambo iliyopo inayotumia gesi asilia ina uwezo wa kuzalisha Megawati 441, lakini huzalisha Megawati 300 kutokana na uhaba wa miundombinu ya kuchakata na kusafirisha hiyo.
Aidha, Serikali inatarajia utendaji mahiri wa EWURA kuwa chachu ya kuboresha utoaji wa huduma za uchakataji na usafirishaji wa gesi asilia hapa nchini, kwani kwa kufanya hivyo itaongeza upatikanaji na ubora wa huduma na kuleta ufanisi endelevu wenye kuzingatia uboreshaji wa mazingira nchini.
“Hii ni miongoni mwa juhudi za EWURA katika kushirikiana na wadau na kupata maoni kuhusu huduma zitolewazo na TPDC pamoja na mipango itakayowasilishwa katika sekta hii muhimu ya Gesi asilia”, aliongeza Mhe. Sadick.
Wito ulitolewa kwa wadau hao kuwa makini, kujenga hoja kushiriki kwa nia njema, pamoja na kutoa maoni yakiwa na lengo la kuhakikisha kuwa mizania kati ya watumiaji huduma za uchakataji na usafirishaji wa gesi asilia inawepo, kwani TPDC na Taifa linafikia malengo ya matumizi ya gesi hiyo katika kukuza uchumi wa nchi.