Saturday, November 22, 2014

Rais Kikwete aomboleza vifo vya waandishi wa habari



Rais Kikwete aomboleza vifo vya waandishi wa habari

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia Salamu za Rambirambi Waziri wa Habari, Vijana Utamaduni na Michezo, Mheshimiwa Dkt. Fenella Mukangara kuomboleza vifo vya Waandishi wa Habari, Innocent Munyuku wa Kampuni ya New Habari (2006) Ltd. na Baraka Karashani ambaye alikuwa Mwanachama wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo nchini.

Mwandishi Mwandamizi, Innocent Munyuku alifariki akiwa usingizini nyumbani kwake Kimara Jijini Dar es Salaam, wakati Baraka Karashani aliaga dunia katika Hospitali Kuu ya Jeshi Lugalo Jijini Dar es Salaam alikokuwa amelazwa kwa matibabu.

"Nimesikitishwa na kuhuzunishwa mno na vifo vya Waandishi hawa kwa vile ni pigo siyo tu kwa Tasnia ya Habari waliyokuwa wanaitumikia na Wanahabari kwa ujumla, bali pia kwa Taifa letu ambalo mchango wao kama Waandishi wa habari ni muhimu kwa maendeleo ya nchi yetu na Taifa kwa ujumla", amesema Rais Kikwete katika Salamu zake.

Rais Kikwete amemwomba Dkt. Fenella Mukangara kumfikishia Salamu zake za pole kwa familia za Wanahabari hao kwa kupotelewa na mihimili na nguzo muhimu za familia zao, lakini amewahakikishia wanafamilia kuwa binafsi yuko pamoja nao katika kuomboleza misiba ya wapendwa wao.

"Namuomba Mwenyezi Mungu awape Wanafamilia wa Waandishi hao moyo wa uvumilivu na subira kipindi hiki wanapoomboleza vifo vya wapendwa wao, na naomba azipokee na kuzilaza Mahala Pema Peponi Roho za Marehemu, Innocent Munyuku na Baraka Karashani, Amina"., amemalizia kusema Rais Kikwete katika Salamu zake.

Imetolewa na:

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,

Ikulu,

DAR ES SALAAM

22 Novemba, 2014