Friday, November 28, 2014

Msanii wa Komedy wa Nigeria awasifu wasanii wa Tanzania



Msanii wa Komedy wa Nigeria awasifu wasanii wa Tanzania
MSANII wa vichekesho (komedy) kutoka Nigeria,Okopcha Bright Onyekere maarufu kama Basket Mouth amewasifu wasanii wa Tanzania kwa juhudi wanazofanya kuelimisha jamii kutumia vipaji vyao.

Akizungumza Dar es Salaam jana baada ya kuwasili kutoka Nigeria kwa ajili ya onesho maalum kushirikiana na wasanii wa Tanzania juzi Dar es Salaam alisema kutoka aanze sanaa ya vichekesho miaka 16 iliyopita amekuwa akipata sifa za wasanii wa Tanzania wakiwika katika fani za muziki, sanaa za filamu, michezo ya kuigiza na vichekesho.

Onyekere aliyetamba nchini Nigeria na Bara la Afrika katika fani hiyo amekuja kufanya onesho moja lililopangwa kufanyika jana hoteli ya Golden Tulip, aliongeza kuwa sanaa ni utajiri mkubwa kama vipaji walivyopewa vitatumika ipasavyo na kutawala jukwaa .

Mkurugenzi wa Kampuni ya Vuvuzela, Evans Bukuku alisema lengo la kumleta msanii huyo wa komedy ni kuimarisha sanaa ya vichekesho kwa wasanii chipukizi wa Tanzania ambao wanahitaji kuandaliwa kwa soko hilo nchini na nje ya nchi.

Alisema Kampuni ya Vuvuzela imejitolea kusaidia wasanii wa vichekesho nchini na kuwafundisha namna watakavyoweza kuendeleza fani hiyo kazi iliyoanza miaka minne iliyopita kampuni ilipoanzishwa.

Bukuku alisema kila mwisho wa mwezi kuna onesho maalum ambalo hutumika kuonesha vipaji vya wasanii wa vichekesho na jinsi msanii anavyoweza kutawala jukwaa kuwaburudisha watazamaji.

Alisema kampuni yake inatarajia kufanya maonesho kama hayo mikoa mbalimbali ya Tanzania kuibua wasanii wengine wenye uwezio katika fani hiyo.

Mkurugenzi Bukuku alisema katika onesho la karibuni Watanzania walikongwa nyoyo zao pale wasanii wa Tanzania washirikiana na wasanii wa vichekesho kutoka Kenya ambaye ni Mdomo Baggy na Dick Omondi kutoka Uganda anayejulikana kama Uncle Bob kufanya onesho kali nchini.

Bukuku aliwashukuru wadhamini waliojitokeza kusaidia kufanyika kwa onesho hilo ambao ni Shirika la Ndege la Afrika Kusini (SAA),Hoteli ya  Golden Tulip, Gazeti la Mwananchi Communications, Clouds Media Group, Ultimate security, Simu TV, Prime Advertising, Dar insites, Advertising Dar, Bongo 5, Eventlites, Hugo Domingo na Michuzi Blog.