Monday, November 03, 2014

MAFUNZO YA ELIMU YA UJASIRIAMALI KWA WASHIRIKI WA SHINDANO LA MASHUJAA WA KESHO MKOANI MTWARA YAMALIZIKA



MAFUNZO YA ELIMU YA UJASIRIAMALI KWA WASHIRIKI WA SHINDANO LA MASHUJAA WA KESHO MKOANI MTWARA YAMALIZIKA
Mafunzo ya elimu na ujasiriamali kwa washiriki wa shindano la Mashujaa wa  Kesho yanayoratibiwa na kampuni ya Statoil Tanzania, yenye lengo la kumjenga  kijana kuwa mjasiriamali yamekamilika hivi karibuni.

Akibainisha aina ya mafunzo ya ujasiriamali waliyopata vijana hao, Erick
Mchome Afisa Mahusiano wa Statoil-Tanzania amesema kuwa
Mafunzo waliyopata vijana hao yamelenga kuwawezesha vijana kuandika mpango wa biashara ikiwa ni hatua ya awali katika harakati za ujasiriamali.

Pamoja na hilo vijana pia wamefundishwa kujenga uwezo wa kujieleza kwani sifa moja ya mjasiriamali ni kujiamini na kuweza kusimama mbele ya wateja kunadi biashara yake. '' Tumekuwa na siku nne nzuri za mafunzo na ni imani yetu kuwa vijana hawa hamsini na ziaidi watakuwa chachu ya mafanikio kwa vijana wenzao kwani mafunzo haya yamewatoa kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine,'' alisema Mchome.

Sambamba na hayo vijana hao ambao walifikia idadi ya hamsini na zaidi wamefundishwa namna ya kujijenga kama wajasiriamali ikiwa ni pamoja na namna za kutafuta mtaji, kupanga mapato na matumizi na pia kutenga faida kwa kila biashara watakayofanya. Lengo la mfunzo haya ni kuchochea ari ya ujasiriamali kwa vijana ambao wameshiriki na kuingia awamu ya pili ya shindano la mashujaa wa kesho. 

Kwa upande vijana waliochaguliwa kuingia hii awamu ya pili wao wamesema kuwa elimu waliyoipata imewafungua macho na kupanua mawazo sana. Majadiliano yamewaonyesha wazi kwamba kuna fursa nyingi sana nje ya kuajiriwa.

"Nawashukuru Statoil-Tanzania pamoja na wasimamizi wa mafunzo haya kwani elimu tuliyopata hapa ni msingi mkubwa kwa sisi kuwa wajasiriamali, kufanya biashara zetu ilitukamate fursa za biashara ambazo zipo mbele yetu. Kuna njia nyingi sana za kutafuta maisha ", Alisema Ally Seleman mshiriki wa shindano la Mashujaa wa Kesho.

Mafunzo ya elimu ya biashara na ujasiriamli yalianza toka tarehe 27 Oktoba
2014 na kuendelea kwa siku nne.Mara baada ya mafunzo hayo kukamilika vijana wamepewa siku 12 za kuaandika mawazo ya biashara na kuyakusanya siku ya jumatano ya tarehe 12 mwezi Novemba ili kuweza kuingia katika awamu ya pili ya mchakato wa kupata washindi wa shindano hili la Mashujaa wa kesho.

Shindano la mashujaa wa kesho lilizinduliwa mnamo mapema mwezi Septemba na linatarajiwa kufika kilele mwanzoni mwa mwezi Desemba ambapo mshindi atajinyakulia kitita cha dola za kimarekani elfu tano kutoka kampuni ya Statoil.