Friday, November 07, 2014

JESHI LA POLISI KANDA MAALUM LAUNDA KAMATI ITAKAYORATIBU KERO ZA WAFANYABIASHARA WA KARIAKOO



JESHI LA POLISI KANDA MAALUM LAUNDA KAMATI ITAKAYORATIBU KERO ZA WAFANYABIASHARA WA KARIOAKOO
Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es salaam limeuda kamati ya pamoja baina ya wafanyabiashara wa soko la Kariakoo na maafisa wa Jeshi hilo ili kuwa na utaratibu sahihi wa kushughulikia kero za uhalifu miongoni mwa wafanyabiashara wazalendo na wageni zinazojitokeza katika soko hilo. 

Kamishna wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam Suleiman Kova ametangaza kamati hiyo alipokuwa akijibu hoja na maswali mbalimbali yaliyoulizwa na baadhi ya wafanyabiashara wa sokoni hapo juu ya baadhi ya kero zinazowakabili  katika mkutano na wafanyabiashara hao uliofanyika katika mtaa wa Kongo na Mchikichini jijini Dar es Salaam jana.

Kamati hiyo itawahusisha maafisa wa Polisi na baadhi ya wafanyabiashara na itaongozwa na Naibu Kamishna wa Polisi SIMON SIRRO kama mwenyekiti. Kaimu Mwenyekiti ni bwana JONSON MINJA ambaye pia ni kiongozi wa wafanyabiashara huku Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Ilala, Kamishna Msaidizi Mwandamizi Mary Nzuki atakuwa mjumbe maalum wa kamati hiyo pamoja na wajumbe wengine. 

Awali katika mkutano huo baadhi ya wafanyabiashara walipata fursa ya kutoa dukuduku/kero zanazowakabiri ili zipatiwe ufumbuzi. Baadhi ya kero zilizoianishwa ni pamoja na Kituo cha Polisi Msimbazi kugeuzwa sehemu ya kukusanyia mapato; kutokuwepo na huduma bora kwa mteja toka askari polisi; n.k.

 Mmoja wa wafanyabiashara HUMFREY SAMBO alihoji uhalali wa mgambo wa jijini kufanya kazi zao bila kufuata sheria za nchi na serikali haichukui hatua? Huku weginne wakitaka wahalifu sugu wanaojulikana kama "KAPERO" wakamatwe kwani wamekuwa kero kwa wafanyabiashara na wateja.

Kwa upande wake mwenyekiti wa wafanyabiashara bwana JONSON MINJA amesema hakuna mfanyabiashara asiyependa kulipa kodi bali ameomba pawe na mfumo shirikishi utakaosaidia kuleta uelewa wa pamoja kwa maslahi ya wafanyabiashara na uchumi wa nchi kwa jumla. Pia ameiomba serikali ione sasa kuwa ni muda muafaka kwa wafanyabiashara wazawa kupewa fursa za kuwekeza nchini hasa katika miradi mikubwa ya kiuchumi ili kujenga uchumi imara wa nchi na kukuza uzalendo miongoni mwa watanzania ambao kwa sasa ni kama haupo.

Akijibu hoja mbalimbali toka kwa wafanyabiashara hao Kamishna Kova amesema mbali na kuunda kamati tajwa pia ametoa maagizo yafuatayo:

Kituo cha Polisi Msimbazi kufanya kazi za kuwahudumia wananchi na si kituo cha kukusanya kodi/ushuru. 

Kikundi cha Polisi jamii kinacholalamikiwa kimevunjwa na kitaundwa kingine kinachohusisha watu makini watakaopatiwa mafunzo ya kuifanya kazi hiyo kwa mujibu wa sheria na taratibu.

Kushauriana na Mkurugenzi wa jiji la Dar es Salaam kuona namna ya kuboresha huduma inayotolewa na askari wa jiji kwa kushirikisha Polisi ili iwe ni yenye tija na inayofuata sheria za nchi kuliko ilivyo sasa.

Pia nawataka vibaka maarufu kama KAPERO kujisalimisha wenyewe vinginevyo watasakwa kwa namna yoyote ile mpaka wapatikane na hatua zichukuliwe dhidi yao. Nia ni kuwafanya wafanyabiashara wa ndani na nje kufanya shughuli zao kwa amani na utulivu 
Aidha, nawaasa wafanyabiashara kuacha mtindo wa kubeba pesa nyingi kiholela kwa sababu ni hatari kwa maisha yao hasa katika kipindi hiki kinachotawaliwa na utandawazi na badala yake watumie mifumo ya kisasa ya kibenki ya usafirishaji fedha ikiwa ni pamoja na kuomba eskoti toka Jeshi la Polisi. 

Mwisho nawataka watanzania kuacha mtindo wa kujichukulia sheria mikononi kwa sababu tabia hii imekuwa ikikatisha maisha ya watu ilihali sheria za haki za binadamu zinakiukwa jambo ambalo si la kizalendo hata kidogo. Ni vema kuachia vyombo husika vikasimamia sheria kwa wale wanaokiuka sheria hizo kuliko kujichukulia sheria mikononi.