Tuesday, November 25, 2014

JAJI MKUU WA TANZANIA MHE MOHAMED CHANDE OTHMAN ATEMBELEA UBALOZI WA TANZANIA, WASHINGTON DC



JAJI MKUU WA TANZANIA MHE MOHAMED CHANDE OTHMAN ATEMBELEA UBALOZI WA TANZANIA, WASHINGTON DC
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Mohamed Chande Othman ametembelea Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania uliopo Washington DC, Marekani, na kufanya mazungumzo na wafanyakazi wa Ubalozi huo Ubalozini hapo Tanzania House. 
Katika mazungumzo yake hayo, Mhe. Chande, ambaye yuko Marekani katika ziara ya kikazi na ujumbe wake,  aliwaeleza watumishi wa Ubalozi namna mihimili mitatu ya dola inavyofanya kazi pamoja na mipaka yake. 
Alibainisha kwamba Tanzania inajivunia mahusiano mazuri yaliyopo baina ya mihimili hiyo ambayo kutokana na misingi thabiti imekuwa ikifanya kazi katika mazingira mazuri yanayojikita katika kulisukuma taifa la Tanzania mbele. 
Mhe. Chande alisema pia Tanzania imo katika juhudi kubwa za kuhakikisha wananchi wake wanapata huduma za kimahakama katika kila ngazi ili kukidhi mahitaji yaliyopo sasa katika mikoa mbali mbali.
Aliongeza kwamba jambo la msingi  kwa sasa ni kuongeza ufanisi katika shughuli za kimahakama na hili linahitaji zaidi rasilimali fedha ili vyombo vyote viweze kutekeleza majukumu yake kwa wakati muafaka.
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Mohamed Chande akisaini kitabu cha wageni katika Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Washington DC, Marekani.
Jaji Mkuu Mhe. Mohamed Chande Othman (wa Tatu Kushoto) katika picha ya pamoja na Maofisa wa Ubalozi wa Tanzania Washington DC na watumishi wengine wakati wa ziara yake Ubalozini na ujumbe wake. Wa nne Kushoto, ni Mhe. Prof. Ibarahim Juma, Jaji wa Mahakama ya Rufaa na wa Pili kulia ni Mhe. Aloysius Mujulizi, Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Mohamed Chande akipewa muhtasari wa shughuli za ubalozi na Mkuu wa Utawala ubalozini hapo Mama Lillian Munanka