Wednesday, November 26, 2014

IPTL:Huku Bunge kule Mahakama



IPTL:Huku Bunge kule Mahakama
Ripoti itakayowasilishwa bungeni hii hapa.
Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) wakiilinda ripoti hiyo usiku kucha.
Wajumbe wa kamati wakiipitia ripoti hiyo kabla ya kuwasilishwa leo bungeni.

Wakati mahakama ikitangaza kuzuia kashfa ya kampuni ya IPTL ya uchotwaji wa zaidi ya Sh. bilioni 300 kwenye akaunti ya Tegeta Escrow, iliyoko Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kujadiliwa na Bunge, Spika wa Bunge, Anne Makinda, amesisitiza kuwa mjadala kuhusu suala hilo utafanyika kama ulivyopangwa.

Makinda amesema kamwe hakuna anayeweza kulizuia Bunge kazi zake za kibunge.

"Msianze kuishi kwa wasiwasi, sisi kinga zetu ziko wazi, hakuna atakayetuzuia kufanya kazi za kibunge na zinazopatikana katika maeneo tunayopita na hatuwezi kushitakiwa," alisema Makinda.

Kwa kauli hiyo ya Spika Makinda, vigogo waliochota, waliofaidika na mgawo na kama taratibu za kisheria za uchotwaji wa fedha hizo kutoka kwenye akaunti hiyo zilifuatwa au la, wanatarajiwa kujulikana leo.

Hiyo ni baada ya ripoti ya uchunguzi wa kashfa ya kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) ya uchotwaji wa fedha hizo kwenye akaunti hiyo, kuanika kila kitu kuhusu kashfa hiyo bungeni leo.

Jana Spika Makinda aliwataka wabunge kujiamini na kujiandaa kwa kusoma ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), iliyotokana na chunguzi wa kashfa ya uchotwaji wa fedha hizo kwenye akaunti hiyo, ili wakidhi haja ya kuchangia mjadala huo leo.

Alisema hayo akijibu miongozo iliyoombwa kwa nyakati tofauti na wabunge; John Cheyo (Bariadi Mashariki-UDP) na John Mnyika (Ubungo-Chadema), bungeni jana.

Cheyo alimuomba Spika Makinda atoe mwongozo ikiwa leo Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) itawasilisha taarifa yake na ripoti ya CAG,kuhusu kashfa hiyo kufuatia kuwapo taarifa kwamba jana ilifunguliwa kesi mahakamani kupinga suala hilo kuingizwa bungeni.

"Naona hii hali inaanza kushamiri nchini, Bunge linapotaka kushughulikia jambo kama muhimili, wanajitokeza watu kwa kutumia ujanja ujanja, wanatumia mihimili mingine kuzuia, naomba mwongozo katika hili," alisema Cheyo.

Makinda alitumia fursa hiyo kuwatangazia wabunge kwamba, jana mchana mara baada ya kuahirishwa bunge, kila mmoja angegawiwa ripoti ya CAG na kwamba ilitakiwa wagawiwe kabla ya bunge kuahirishwa lakini ilikuwa bado inadurufiwa.

Makinda alikiri kuwa na taarifa zilizoelezwa na Cheyo, alisisitiza kuwa wana orodha ya kesi zote zilizopo mahakamani, ambazo zinahusu IPTL hakuna hata moja inayohusu kitakachojadiliwa leo bungeni.

Mnyika pamoja na kumpongeza Makinda kwa kusema Bunge lazima lipelekewe na kujadili ripoti hiyo, alimtaka Spika Makinda kuwahakikishia kuwa hata kesi iliyofunguliwa jana na kampuni ya Pan African Power (PAP), haitapewa nafasi ya kuzima 'moto' huo kuwaka bungeni.

"Umesema hakuna kesi yoyote…, nakupa taarifa mahususi kuwa PAP, leo (jana) wamefungua kesi kwenye Mahakama Kuu ya Tanzania wakiomba Bunge lizuiwe kujadili suala la Escrow, tunaomba utuhakikishie hili halitatokea," alieleza Mnyika.

Spika Makinda alisisitiza kuwa bunge ni muhimili, unaoendesha shughuli zake kwa uhuru na lina kinga na haki zake.

Alisema ikitokea mtu au chombo chochote kuamua bunge lifanye au lisifanye nini, hilo halitakuwa bunge tena.

Hata hivyo, Makinda alishindwa kuwahakikishia wabunge kuwa leo watajadili Escrow kwa maelezo kwamba, hakuwa amepokea taarifa ya maandishi kutoka PAC kama taratibu zinavyoelekeza.

MAAMUZI YA MAHAKAMA
Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, imezuia Bunge kujadili ripoti ya CAG kuhusu uchunguzi wa kuchotwa kwa zaidi ya Sh. bilioni 300 katika akaunti ya Tegeta Escrow iliyopo BoT hadi hapo Mahakama itakaposikiliza shauri la msingi Desemba 8, mwaka huu.

Mahakama hiyo ilitoa uamuzi huo baada ya kuridhika na maelezo yaliyotolewa na kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) na kampuni tanzu ya Pan African Power, kufuatilia hati yao ya dharura namna 51 ya kusitishwa kwa mjadala huo, iliyowasilishwa Mahakamani hapo jana.

Hati hiyo ya dharura ilisikilizwa na majaji watatu ambao ni Radhia Sheikh akisaidiana na wenzake Richard Mziray na Lugano Mwandambo kuanzia saa 8:45 hadi saa 10:45.

Jopo la Mawakili upande wa watoa maombi ya hati ya dharura liliongozwa na Joseph Makandege akisaidiana na wenzake, Gabriel Mnyele na Felician Kay.

Upande wa watoa maombi, uliiomba mahakama hiyo kusitisha mjadala huo kwa maelezo kwamba mhimili wa Bunge unahusika na utungaji wa sheria, hivyo kujadili mashauri yanayohusu kesi za jinsi hiyo ni kuingilia uhuru wa mhimili mwingine ambao ni Mahakama.

Makandege alidai kuwa ni kweli Bunge lina kinga ya kujadili suala kama hilo kwa mujibu wa ibara ya 100, lakini ikiwa suala hilo likiwa katika ofisi ya Bunge.
Alidai kuwa Bunge likiendelea kujadili kutasababisha mashauri ya IPTL na PAP yaliyoko Mahakama Kuu na Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi yataminywa na kunyimwa haki yao.

BUNGE: MJADALA LEO
Baada ya Mahakama kutangaza maamuzi hayo, Kaimu Katibu wa Bunge, John Joel, aliliambia NIPASHE kuwa hawajapokea taarifa kwamba Mahakama ni mhimili na Bunge ni mhimili mwingine, hivyo wataendelea na na mjadala.

Wakati huohuo; mtu aliyekamatwa mwishoni mwa wiki iliyopita na jeshi la polisi mkoani Dodoma, akituhumiwa kusambaza nyaraka zinazosadikiwa kuwa ni ripoti ya CAG, bado anaendelea kushikiliwa.
Nyaraka hizo, zilidaiwa kuibwa kutoka kwenye Ofisi ya Katibu wa Bunge kabla ya kupatikana zikisambazwa mitaani na mtuhumiwa huyo, kabla hajakamatwa.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, David Misiime, alilieleza Nipashe jana kuwa kutokana na sababu za kiupelelezi, utambulisho wa mtuhumiwa bado unaendelea kuhifadhiwa.
"Siwezi kueleza upelelezi utakamilika lini, sasa tunaendelea kutumia wataalam wa maandiko ili kujiridhisha ikiwa nyaraka hizi ni za CAG au la, tukikamilisha kazi zetu tutatoa taarifa," alisema Kamanda Misime.

KAFULILA ATISHIWA KIFO
Wakati hayo yakijiri, Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila, alitumiwa ujumbe mfupi wa simu ya mkononi (sms) unaomtishia maisha.

Sehemu ya sms hiyo inasema: "Nadhani umeamua kifo kwa kutafuta sifa za kijinga nakuhurumia sana kwa kuwa hujui unapambana na nani huu ni ujumbe wa mwisho kwako kama huamini utaamini ukiwa kaburini."

Kutokana na hali hiyo, jana Kafulila alikwenda makao makuu ya polisi mkoani Dodoma kutoa taarifa dhidi ya vitisho hivyo.

Alifuatana na wabunge; Khatib Said Haji (Konde-CUF), Mohammed Habib Mnyaa (Mkanyageni-CUF) na Moses Machali (Kasulu Mjini-NCCR-Mageuzi).Hata hivyo, Kamanda Misime alisema jana kuwa hakuwa na taarifa zozote kuhusiana na malalamiko hayo.

RIPOTI
Ripoti hiyo inatarajiwa kuwasilishwa kupitia taarifa maalum ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) na Mwenyekiti wake, Zitto Kabwe, pamoja na mapendekezo ya kamati hiyo leo.

Ripoti hiyo inahusu ukaguzi wa hesabu za fedha hizo uliofanywa na CAG kwa upande mmoja na uchunguzi uliofanywa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru) kwa upande mwingine, kuhusiana na kashfa hiyo.

Uchunguzi huo ulifanywa na taasisi hizo kufuatia agizo la Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alilolotoa bungeni, akitekeleza azimio lililopitishwa na Bunge kuhusiana na suala hilo.

Baada ya Zitto kuwasilisha taarifa maalum kuhusiana na ripoti hiyo, wabunge watapata fursa ya kuijadili.

Mjadala huo kama utafanyika unatarajiwa kuliteka Bunge kutokana na sababu mbalimbali, ikiwamo wingi wa fedha hizo zinazodaiwa kuchotwa kifisadi.

Fedha hizo zinadaiwa kuwa ni za umma na kwamba zingeweza kujenga miradi mingi ya maendeleo, ikiwamo ujenzi wa zahanati, ununuzi wa dawa hospitalini, ujenzi wa shule nakadhalika.

Fedha hizo zinadaiwa kuchotwa kutoka kwenye akaunti hiyo ya Escrow na vigogo mbalimbali, wakiwamo mawaziri, wabunge, majaji wa Mahakama Kuu na viongozi wa dini.
Tayari wabunge walianza kugawiwa nakala ya ripoti hiyo jana mchana ili wapate fursa ya kuipitia kabla ya kuijadili bungeni.

Spika Makinda aliliambia Bunge jana kuwa nakala za ripoti hiyo, ambazo wamegawiwa wabunge jana, ni kama kiambatanisho cha taarifa maalum inayotarajiwa kuwasilishwa na PAC leo.

Kabla ya ripoti hiyo kugawiwa wabunge, Jumapili wiki iliyopita, Jeshi la Polisi liliwatia mbaroni vijana wawili kwa tuhuma za kuiiba kutoka Ofisi ya Katibu wa Bunge.
CHANZO: NIPASHE