*Ni wa kujenga maghala makubwa ya kuhifadhia chakula.
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema Serikali inaangalia uwezekano wa kupata mkopo wenye masharti nafuu kutoka Serikali ya Poland utakaoliongezea Taifa uwezo wa kuhifadhi chakula tofauti na hali ilivyo sasa.
Alisema uzalishaji mwaka huu umetoa ziada ya tani milioni 1.5 za nafaka na tani 800,000 za mpunga ikilinganishwa na ziada ya tani 300,000 iliyokuwepo mwaka jana. "Serikali inakabiliwa na changamoto ya kupata soko la uhakika kwa mazao ya wakulima kwa sababu tulizoea kumtumia Wakala wa Hifadhi ya Taifa ya Chakula (NFRA) kama mnununzi mkuu na uwezo wezo wake ni tani 240,000 tu kwa mwaka," alisema.
Akizungumza baada ya kutembelea kampuni ya MLYNPOL ambayo inanunua mazao kwa wakulima na kusindika nafaka jana mchana (Ijumaa, Oktoba 24, 2014) Waziri Mkuu alisema teknolojia ya ujenzi wa maghala makubwa ya kuhifadhia chakula katika muda mfupi ndiyo suluhisho pekee kwa wakulima wa Tanzania katika kipindi tulichonacho.
"Wenzetu wana teknolojia ya kisasa ya ujenzi wa SILOS (maghala makubwa ya kuhifadhia chakula) pamoja na namna bora ya kuhifadhi chakula, na sisi tuna changamoto ya kuwasadia wakulima kuuza mazao kutokana na uzalishaji mkubwa wa nafaka ambao umetokea mwaka huu," alisema.
Alisema ni mapema mno kujua kiasi cha fedha ambacho Serikali inatarajia kukopa lakini alithibitisha kwamba atatuma timu ya wataalamu kutoka sekta husika ili wafanye mazungumzo rasmi na Serikali ya Poland na kukamilisha taratibu za upatikanaji wa mkopo huo.
Waziri Mkuu ambaye alisafiri km. 500 kwenda mji wa CHOJNOW kilipo kiwanda cha kutengeneza maghala (SILOS) na kusindika nafaka aliguswa na teknolojia inayotumika kwenye kiwanda hicho cha MLYNPOL ambapo kwa siku moja kina uwezo wa kusindika tani 360,000.
Mji wa CHOJNOW upo kusini Mashariki mwa Poland na pia hauko mbali na mipaka ya nchi za Ujerumani, Czeck na Austria. Kwa gari dogo ni kati ya saa 3 hadi 4 hadi kufika miji mkuu ya nchi hizo ambayo ni Berlin, Prague na Vienna.
Akitoa maelezo kwa Waziri Mkuu, mmiliki wa kiwanda hicho kikubwa nchini Poland, Bw. WITOLD KARCZEWSKI alisema kiwanda hicho kinaposindika ngano kina uwezo wa kutoa unga laini wa mikate (refined flour), unga wa lishe (grain/brown flour), unga wa kutengeneza pasta na tambi na wa mwisho hutolewa kwa ajili ya chakula cha mifugo.
"Nafaka zikifika, zinasafishwa, zinakaushwa, zinapimwa unyevunyevu uliopo na kuanza kusindikwa kulingana na aina ya nafaka inayoletwa. Tunakusanya mazao haya kutoka kwa wakulima kwenye majimbo 16 ya nchi hii," alisema.
Akifafanua kuhusu matumiai ya umeme kwenye kiwanda hicho, Bw. ALEKSANDR ZINGMAN ambaye pia ni mshauri na mbia wa Bw. KARCZEWSKI, alisema kiwanda hicho kinatumia megawati moja ya umeme kwa saa moja lakini matumizi yanaweza kupungua kuligana na ukubwa ama udogo wa kiwanda. "Kama Serikali inahitaji kiwanda kidogo zaidi ya hapa, tunaweza kuwajengea na matumizi ya umeme lazima yatapungua," alisema.
Kampuni ya MLYNPOL ina wafanyakazi 250 ambao kato yao, 200 wanafanya kazi kiwandani kwa shifti tatu za saa nane nane kila moja. Waziri Mkuu anamalizia ziara yake ya siku tatu nchini Poland jana mchana ambapo asubuhi alikutana na Watanzania waishio Poland na baadaye kufanya vikao na baadhi ya wafanyabiashara wa jiji la Warsaw.