WATU watano wamekamatwa jijini Dar es Salaam wakiwa na kilo saba za dawa za kulevya aina ya heroin zenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 315 wakiwa wanazifungasha kwa ajili ya kuzisafirisha.
Kamanda wa Polisi wa Kikosi Maalumu cha Kupambana na Kuzuia Dawa za Kulevya nchini, Godfrey Nzowa alisema watuhumiwa hao walikamatwa usiku wa kuamkia jana Magomeni Mapipa katika Manispaa ya Kinondoni.
Aliwataja wanaoshikiliwa kuwa ni Muharami Mohamed maarufu kama Chonji (44), Malik Zuberi (29), Tanaka Adam (35), Rehani Mursal (45), Abdul Abdallah (37), wote wakazi wa Magomeni Mapipa.
"Watuhumiwa hawa walikamatwa wakiwa na kilo saba za heroin wakiwa wanazifungasha tayari kwa ajili ya kuzisafirisha. Pia tuliwakuta wakiwa na mizani ambayo walikuwa wakiitumia kupima dawa hizo za kulevya," alisema.
Alisema kukamatwa kwa watuhumiwa hao kunatokana na ushirikiano walioupata kutoka kwa raia wema ambao wamekuwa mstari wa mbele kutoa taarifa katika jeshi hilo pale wanapogundua kuna uhalifu.
Aidha alisema mpaka sasa bado haijajulikana watuhumiwa hao walikuwa wanataka kuzisafirisha dawa hizo kwenda nchi gani. Wanashikiliwa kwa mahojiano zaidi.
HABARI LEO