Saturday, October 25, 2014

WATOTO WALEMAVU MAHENGE WANUFAIKA NA MSAADA WA BAISKELI



WATOTO WALEMAVU MAHENGE WANUFAIKA NA MSAADA WA BAISKELI
 Mtoto Mwidini Ligubuga kutoka kijiji cha Mbuga akifurahia kiti chake kutoka kwa Kibaran Resources . Kushoto ni Mkurugenzi wa kampuni hiyo nchini Bw.  Grant Pierce, na kulia ni Mkurugenzi Mkuu  Bw. Andrew Spinks 


 Kaimu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mahenge Bw. Furaha Lilongeri akimbeba Mtoto Magdalena Nwira kutoka kijiji cha Kichanganyi kupokea kiti chake. Mkurugenzi wa Kibaran Resources Grant Pierce anasaidia kukitayarisha hicho kiti.
Watoto Mahenge wakipokea viti kutoka kwa kampuni ya Kibaran Resources 
Kampuni ya Kibaran Resources inayojihusisha na utafiti wa uchimbaji wa madini ya Uno kwenye Kijiji cha Epanko, imetoa msaada wa baiskeli 30 za walemavu kwa watoto wenye ulemavu katika kata ya Mahenge wilaya ya Ulanga mkoani Morogoro. Baiskeli hizo zimeundwa maalumu kwa watoto wanaoishi vijijini. 

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kukabidhi baiskeli hizo, Bw. Grant Pierce, ambaye ni mkurugenzi wa kampuni ya Kibaran Resources Tanzania amesema kuwa msaada huo ni sehemu ya miradi ya maendeleo ya kijamii ambayo kampuni imeazimia kuifanya kulingana na msimamo wa kampuni hiyo wa kuwa karibu na jamiii inayowazunguka. 
"Msaada huu ni sehemu ya azimio tuliloweka la kuwekeza katika jamii zinazotuzunguka. Watu wanaoishi na ulemavu husahaulika katika jamii na hawapati haki zote zinazostahili kwa binadamu. Haki za binadamu ni sawa kwa watu wote bila kujali ulemavu wao. Kukosa uwezo wa kujihudumia mwenyewe, huleta mateso kwa binadamu hasa watoto. Tunafurahi kuwasaidia watoto katika jamii hii kwa kuwapa uwezo wa kutoka sehemu moja na kwenda sehemu nyingine kwa urahisi na tunaamini itasaidia kuboresha maisha yao ya kila siku.", Alisema Grant Pierce. 
Naye kaimu Mwenyekiti wa Halmashauri Furaha Lilongeri akimwakilisha Mkuu wa Wilaya  Mh. Francis Miti  kama mgeni rasmi wakati wa shughuli hiyo ya kukabidhi baiskeli za walemavu kwa watoto alisema kuwa amefurahishwa na moyo wa kampuni  hiyo kwa kujali jamii inayoizunguka haswa kundi hilo la walemavu katika wilaya. 
"Nimefurahishwa sana na kitendo cha Kibaran Resources kujitolea katika kuwasaidia watoto hawa. Kwa niaba ya Wilaya, napenda kuushukuru uongozi pamoja na wafanyakazi wote wa Kibaran Resources kwa moyo wenu wa kujali watu walio katika mazingira magumu, ikiwemo watoto wenye ulemavu. Msaada huu utawawezesha watoto hawa kushirki shughuli mbalimbali katika jamii pamoja na kufikia malengo yao, kama vile kwenda shule kama watoto wengine ili kujipatia elimu ambayo ni msingi wa maisha yao.", alisema bwana, Furaha Lilongeri.

Wakizungumza kwa niaba ya watoto wao, walezi wa watoto waliopewa baiskeli hizo wametoa shukurani kwa uongozi wa kampuni ya Kibaran Resources kwa kuwasaidia watoto wao kutimiza ndoto zao za kushiriki katika fursa zilizopo kwenye jamii sawa na watoto wengine wasio na ulemavu. 
"Naishukuru sana kampuni ya Kibaran. Msaada huu tumeupokea kwa furaha kubwa kwani watoto wetu sasa watapata uhuru ambao hawakuwa nao awali. Kwa sisi walezi, hii ni ahueni kubwa sana. Ni vigumu mara nyingine kwa watu kuelewa changamoto ya kulea mtoto mwenye ulemavu. Baiskeli kama hizi zinaondoa mzigo mkubwa sana kwetu". Alisema Anton Nkawamba, mmoja wa walezi waliohudhuria shughuli hiyo. 
Baadhi ya viti viliachwa katika hospitali ya mkoa ili kusaidia watoto wagonjwa wenye ulemavu wakati wanahudhuria hospitali hiyo kwa huduma za matibabu. Viti hivyo hutengenezwa na Shirika la nchini Australia liitwalo Wheelchairs for Kids, shirika ambalo wafanyakazi wake ni wastaafu wanaojitolea.  
Kibaran Resources ni kampuni iliyosajiliwa kwenye soko la hisa la Australia inayojihusisha na biashara ya uchimbaji wa madini aina ya UNO (Graphite) na Nickel nchini Tanzania. Kwa sasa shughuli za Kibaran zimejikita katika eneo la Epanko jirani na Mahenge, Wilayani Ulanga katika mkoa wa Morogoro. Kampuni hiyo imekuwa ikifanya utafiti wake kwa takribani miaka mitatu katika eneo la Mahenge na pia ina mradi katika eneo la Merelani, Kaskazini Mashariki mwa Tanzania. 
Mnamo tarehe 20/08/2014 kampuni ya Kibaran Resources ilitoa msaada wa madawati 148 katika shule ya Epanko iliyokuwa inakabiliwa na upungufu wa madawati na hivyo kutoa fursa kwa wanafunzi 292 kufanya kazi zao za darasani wakiwa wamekaa. Kibaran Resources iko katika utafiti wa kujenga mgodi katika eneo la Epanko. Mgodi huo utatengeneza nafasi za ajira kwa wakazi wa eneo hilo na hivyo kupunguza tatizo la ajira katika mkoa huo.