Friday, October 24, 2014

Ukarabati na Upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Mpanda wakamilika



Ukarabati na Upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Mpanda wakamilika
Serikali imekamilisha ukarabati na upanuzi wa uwanja wa ndege wa Mpanda, mkoa wa Katavi na hivyo kuufanya uwe wa kiwango kizuri tayari kwa kutumika kwa ndege za binafsi na biashara.

Meneja wa Uwanja wa Ndege wa Mpanda, Bw Seneti Lyatuu alisema uwanja huo umeboreshwa na hivyo, unaweza kutumika kutua na kuruka ndege za kiwango cha kati na hata zile ndege kubwa zinaweza kutua kwa dharura.

Aliiambia timu ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo kutoa Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango iliyotembelea uwanja huo mwishoni mwa wiki kuwa uwanja huo umeongeza idadi ya wasafiri mara dufu kutokana na ukarabati na upanuzi uliofanyika.

Meneja wa Uwanja huo alisema idadi ya abiria imeongezeka kutoka abiria 285 mwaka 2009 hadi 2,390 mwaka 2013/14.

Bw. Lyatuu alisema kuwa uwanja huo umekarabatiwa na barabara ya kuruka na kutua ndege imerefushwa kwa kiwango cha lami kutoka urefu wa mita 1,500 na upana wa mita 30 hadi kufikia urefu wa mita 1,820 na upana wa mita 30.

Alisema maeneo mengine yaliyokarabatiwa ni pamoja na kujenga uzio na mifereji ya kupitishia maji ya mvua. "Kwa sasa kiwanja kipo vizuri na ndege za aina zote zinaweza kutua hapa uwanjani hivyo, tunawakaribishwa wadau wote kuutumia uwanja huu" alisema Bw Lyatuu.

Eng. Caroline Mntambo kutoka Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Makao Makuu Dar es Salaam alisema kuwa tayari wamealika mashirika ya ndege yanayofanya biashara hapa nchini kuanzisha safari katika uwanja huo. Mashirika hayo ni pamoja na ATC, Precision Air, Fast jet nk.

Eng Mntambo alisema kwa sasa shirika la ndege la Auric Air tayari limeanzisha safari za kwenda Mpanda ambapo linasafirisha abiria kutoka Dar- Mpanda – Mwanza mara tatu kwa wiki.

Alisema ndege zingine zinazotua uwanjani hapo kwa sasa ni pamoja na za UNHCR, ndege za kukodi na ndege za serikali.
Meneja wa Uwanja wa ndege wa Mpanda, Mkoa wa Katavi Seneti Lyatuu akiwaonesha timu ya ukaguzi wa miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango upanuzi wa uwanja wa ndege wa Mpanda. Nyuma yake (mwenye suti nyeusi) ni Mhandisi Caroline Mntambo kutoka Mamlaka ya Viwanja vya Ndenge Tanzania, Makao Makuu, Dar es Salaam.
Meneja wa Uwanja wa Ndege wa Mpanda Bw. Seneti Lyatuu akifafanua jambo wakati timu ya ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango walipotembelea kiwanja hicho.
Timu ya ukaguzi ikitazama barabara ya kutua na kurukia ndege katika uwanja wa ndege wa Mpanda.
Barabara ya kutua na kurukia ndege katika uwanja wa ndege wa Mpanda, mkoani Katavi.
Mhandisi Caroline Mntambo (mwenye suti nyeusi) akifafanua jambo kwa timu ya wakaguzi kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango. Uwanja wa ndege wa Mpanda umekarabatiwa na kupanuliwa hivyo , kuwa katika hali nzuri kwa matumizi ya ndege zote za binafsi na biashara. PICHA NA JOYCE MKINGA