Thursday, October 23, 2014

shirika la ndege la flydubai lakaribishwa rasmi visiwani Zanzibar



shirika la ndege la flydubai lakaribishwa rasmi visiwani Zanzibar
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba mafungamano yaliyopo ya Kibiashara baina ya Zanzibar na Mataifa ya Ghuba na Mashariki ya mbali yatazidi kuimarika kufuatia kuongezeka kwa mawasiliano ya safari za anga kati ya pande hizo mbili. 
Balozi Seif alisema hayo wakati akizindua safari za anga kati ya Dubai na Zanzibar zilizoanzishwa rasmi na Kampuni ya Kimataifa ya usafiri wa ndege ya Flydubai hafla iliyofanyika katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Amani Abeid Karume Zanzibar. 
Alisema wafanyabiashara wengi wa Zanzibar pamoja na Mwambao wa Afrika Mashariki wamekuwa wakilitegemea sana soko la Dubai ambalo ndilo wanalolitumia kwa kupata biadhaa zao. Balozi Seif alieleza kwamba uanzishwaji wa safari hizo za moja kwa moja kati ya Dubai na Zanzibar utakuwa kiungo kizuri kwa wafanyabiashara hao kuendeleza biashara zao kwa kiwango kikubwa zaidi. 
Akitoa taarifa ya Kampuni ya usafiri wa ndege ya Flydubai Makamu wa Rais wa Kampuni hiyo Bwana Sudhir Screedhara alisema kampuni yake tayari inaendelea kutoa huduma kwa karibu Miji 12 ya Mataifa ya Bara la Afrika. 
Bwana Sudhir alisema mradi wao unaotumia ndege mpya za kisasa aina ya Boeing zipatazo mia moja umewekeza kiwango cha fedha karibu Dola za Kimarekani Milioni Sitini (U$ 60,000,000). 
Mapema Katibu Mkuu Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano Zanzibar Dr. Juma Malik Akil alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara inayohusika na Mawasiliano itakuwa makini katika kuhakikisha miradi yote inayohusu sekta hiyo inasimamiwa vyema. 
Ndege ya Kampuni ya Flydubai ilitua kwenye uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Amaani Abeid Karume Saa 8.00 kamili mchana na kurushiwa maji na gari za Kikosi cha Zimamoto na Uokozi Zanzibar kama ishara ya kukaribishwa rasmi Zanzibar.
 Makamu wa Pili wa Rais na Mgeni wake Makamu wa Rais wa Kampuni ya Kimataifa ya Flydubai Bwana Sudhir Sreedhara aliyevaa miwani wakiangalia burdani ya ngoma ya Utamaduni Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Zanzibar mara baada ya ndege ya Kampuni hiyo kutua kuanzai safari zake kati ya Dubai na Zanzibar.
 Makamu wa Rais wa Kampuni ya Flydubai Bwana Sudhir Sreedhara akimkabidhi nembo ya jambia kama zawadi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif katika hafla ya uzinduzi wa safari za ndege za Kampuni hiyo kati ya Dubai na Zanzibar. Nyuma ya Balozi Seif ni Naibu Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano Zanzibar Mh. Issa Haji Ussi Gavu
 Balozi Seif akimpongeza Makamu wa Rais wa Flydubai Bwana Sudhir Sreedhara kwa auamuzi wa kampuni yake kutoa huduma za usafiri wa ndege kati ya Dubai na Zanzibar. Kati kati yao ni mratibu wa Kampuni  ya Kimataifa ya usafiri wa anga ya Flydubai Bwana  Riyaz Jamal na kushoto ni Balozi mdogo wa Tanzania Dubai, Mhe Omari Mjenga.
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwa katika picha ya pamoja na Uongozi wa Kampuni ya Kimataifa ya Flydubai mara baada ya ndege ya kampuni hiyo kutua kwenye uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Zanzibar kuanza safari zake kati ya Dubai na Zanzibar.Wa mwanzo kulia ni Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mh. Pandu Ameir Kificho akifuatiwa na Balozi Mdogo wa Tanzania Dubai Mhe Omari Mjenga. 
Picha na Hassan Issa wa OMPR – ZNZ.