Friday, October 24, 2014

Mh. Ummy Mwalimu azitaka Halmashauri zote nchini kutoa elimu kwa wananchi juu ya utunzaji wa mazingira



Mh. Ummy Mwalimu azitaka Halmashauri zote nchini kutoa elimu kwa wananchi juu ya utunzaji wa mazingira
Halmashauri zote Nchini zimetakiwa kuendelea kuhamasisha na kutoa Elimu kwa Wananchi juu ya utunzaji wa mazingira na pia kuimarisha miundombinu ya masoko ambayo ni mibovu na ya kizamani.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mheshimiwa Ummy Mwalimu wakati alipofanya ziara ya kutembelea masoko ya manispaa za Temeke na Ilala za jijini Dar es Salaam.

Amekumbushia pia kila Manispaa kuzingatia agizo la Makamu wa Rais la kufanya usafi kila jumamosi ya mwanzo wa mwezi pia ametoa wito watu kutooneana aibu katika kutupa taka hovyo. Kila mtu awe mlinzi wa mwenzie kuhakikisha anatunza mazingira ianavyotakiwa na pia hatupi taka hovyo, alisema Mheshimiwa Ummy.

Katika ziara hiyo aliongea na wafanyabiashara katika masoko hayo na walimwambia changamoto wanazokutana nazo katika swala zima la kudumisha usafi katika sehemu zao za biashara ni uhaba wa maji na vifaa vya kufanyia usafi.

Ziara hiyo ni muendelezo wa ziara za mbalimbali za Viongozi wa Ofisi ya Makamu wa Rais katika kuhakikisha utunzaji wa Mazingira unafanikiwa kwa kiasi kikubwa katika jiji la Dar es Salaam na Nchi ya Tanzania kwa ujumla.
Naibu Wazir Ofisi ya Makamu wa Rais Mheshimiwa Ummy Mwalimu akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni Injinia Mussa Natty.
Naibu Wazir Ofisi ya Makamu wa Rais Mheshimiwa Ummy Mwalimu akipata maelezo juu ya usafi wa mazingira eneo la soko unavyofanyika. Anayetoa maelezo ni Mwenyekiti wa Soko la Tandale Sultan Ally Kinombo.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Mheshimiwa Ummy Mwalimu (katikati) akiwa katika ziara kukagua soko la Temeke la Stereo. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Temeke Protidas Kagimbo.