Na. Ally Mataula – Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
Meya wa Halmashauri Manispaa ya Tabora Mhe. Gulam Hussein Dewji Remtullah amefikishwa mbele ya Baraza la Maadili kujibu tuhuma zinazomkabili.
Akisoma hati ya malalamiko mbele ya Mwenyekiti wa Baraza hilo Mhe. Jaji (Mst.) Hamisi Msumi, Mwanasheria wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Bw. Hassan Mayunga alilieleza Baraza hilo kuwa Mlalamikiwa akiwa Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora kwa makusudi kabisa alikiuka Maadili ya Viongozi wa Umma kwa kukiuka kifungu cha 6(a) na (d), 12(1) na 15 (b) vyote vya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na. 13 ya mwaka 1995.
Bw. Mayunga alilifafanulia Baraza kuwa Mhe. Gulam Hussein Dewji analalamikiwa kwa kujinufaisha binafsi kwa kutumia fedha kiasi cha shilingi 2,672,000/= mali ya Halmashauri ya Manispaa ya Tabora kwa ajili ya safari ya nchini Marekani huku safari hiyo ikiwa imedhaminiwa na kugharamiwa na Wadhamini waliomualika kutembelea nchini Marekani mnamo Mwezi Aprili, 2011. Pia, Mhe Gulam Dewji analalamikiwa kuvunja Sheria ya Maadili makusudi kwa kipindi cha miaka minne yaani kuanzia mwaka 2010 hadi 2013 kwa kutoa Tamko la uongo kwa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma huku akijua kuwa ni kosa kufanya hivyo.
Kosa lingine analolalamikiwa Mhe. Gulam Dewji ni kushindwa kutamka rasilimali zake ambazo ni pamoja na viwanja Na. 100 kitalu G, 158 Kitalu G, 637 kitalu D, 99 kitalu F, 206 kitalu C pamoja na nyumba moja iliyopo kwenye kiwanja Na. 42 kitalu G vyote vikiwa katika Manispaa ya Tabora. Aidha, Mali nyingine anazodaiwa kushindwa kuzitamka Mhe. Gulam Dewji ni pikipiki 422, duka moja, magari namba T 327 ADS Toyota Hilux, T 842 AWR Toyota Rav4, na T 110 CMW Toyota Rav4.
Bw. Mayunga alimaliza kumsomea hati ya malalamiko Mhe. Gulam Dewji kwa kulieleza Baraza kuwa kwa kufanya hayo na kushindwa kutekeleza majukumu yake kwa uadilifu ni ukiukaji wa maadili ya viongozi wa umma kwa mujibu wa kifungu cha 6(a) na (d), 12(1) na 15(b) vyote ni vya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
Aidha, Bw. Mayunga aliliomba Baraza la Maadili lenye mamlaka ya kisheria ya kufanya uchunguzi wa kina na kumtaka mlalamikiwa kutoa taarifa bayana kuhusu rasilimali zake na kutoa hati na kumbukumbu ambazo ziko chini ya udhibiti wake kuhusu rasilimali hizo kabla ya hatua nyingine kuchukuliwa kwa mujibu wa sheria.
Naye Shahidi wa upande wa walalamikija Bw. Gerald Mwaitebele ambaye ni Mtumishi wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kanda ya Magharibi - Tabora alilieleza Baraza la Maadili kuwa Ofisi ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma – Kanda ya Magharibi Tabora walipata tuhuma saba za ukiukaji wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma dhidi ya Mlalamikiwa kupitia vyombo vya habari.
Bw. Mwaitebele aliendelea kulieleza Baraza hilo kuwa baada ya kufanya uchunguzi wa awali walifanikiwa kupata ushahidi kwa malalamiko matatu na mengine hawakuweza kupata ushahidi na hivyo kuamua kuyaacha.
Kwa mujibu wa Bw. Mwaitebele tuhuma ambazo waliweza kupata uthibitisho baada ya uchunguzi wa awali ni pamoja na kutumia madaraka vibaya kwa kujinufaisha fedha za Halmashauri ya Manispaa ya Tabora, kutumia vibaya madaraka kwa kujitwalia mali ambazo ni viwanja na kutoa tamko la uongo kwa kushindwa kutaja mali zake yeye binafsi, mke pamoja na watoto wake.
Hata hivyo Mlalamikiwa Mhe. Gulam Hussein Dewji alikana malalamiko yote dhidi yake na Mwenyekiti wa Baraza la Maadili Mhe. Jaji (Mst.) Hamisi Msumi aliahirisha kusikiliza shauri hilo hadi tarehe nyingine itakayotangazwa hapo baadae.
Baraza la Maadili ni chombo cha kisheria chini ya fungu la 26 la Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma lenye mamlaka ya kufanya uchunguzi wa kina kuhusu malalamiko yanayohusu ukukaji wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma dhidi ya kiongozi yeyote.
Kwa mujibu wa fungu la 26 (8) linasema kuwa katika taarifa yake, Baraza linaweza kutoa mapendekezo kuhusu hatua za kiutawala, mashitaka ya jinai au hatua nyingine zozote za kuchukuliwa dhidi ya kiongozi husika kwa kadri litakavyoona inafaa.
Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora Mhe. Gulam Hussein Dewji (aliyeshika chupa ya maji) akizungumza na Waandishi wa Habari mara baada ya kutoka kuhojiwa na Baraza la Maadili juu ya tuhuma zinazomkabili kuhusu ukiukaji wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma katika Ukumbi wa Karimjee, Jijini Dar es Salaam.
Shahidi upande wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Bw. Gerald Mwaitebele kushoto akizungumza na Mwanasheria wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Bw. Filotheus Manula mara baada ya kutoa ushahidi wake kuhusu tuhuma za ukiukaji wa Sheria ya Maadili zinazomkabili Meya wa Manispaa ya Tabora Mhe. Gulam Dewji mbele ya Baraza la Maadili katika Ukumbi wa Karimjee, Jijini Dar es Salaam.