Monday, October 27, 2014

Mbio za Rock City 2014 zatia fora



Mbio za Rock City 2014 zatia fora
Wakimbiaji kutoka makampuni mbalimbali na walemavu wa ngozi (albino) wakichuana katika Mbio za Rock City Marathon (Kilomita 5) zilizowahusisha walemavu wa ngozi na watu kutoka makampuni mbalimbali Jijini Mwanza Jana.
washindi wa mbio za watoto wakiwa katika picha ya pamoja na Rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Andrew Mtaka, wakifurahi na bahasha zao za zawad.
Mshiriki wa km 21 akimaliza mbio hizo.
mshiriki wa km 21 akiweka alama kwenye vidole alipofika eneo la samaki jijini mwanza.
Meneja Kiongozi wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) Mwanza, Bw. Hamis Faki (wa pili kushoto) akitoa hotuba wakati wa kuhitimisha Mbio za Rock City Marathon zilizofanyika jijini Mwanza Jana.
 Katibu Mkuu wa Chama cha Riadha nchini Suleiman Nyambui,akiwapa maelekezo wakimbiaji wa Km 21, kabla ya mbio kuanza,kwenye uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza
Meneja Kiongozi wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) Mwanza, Bw. Hamis Faki (wa kwanza kushoto) na Rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania, Bw. Andrew Mtaka (wa tatu kushoto), wakiwa katika picha ya pamoja na washindi wa Mbio za Rock City Marathon 2014 (Kilomita 21) upande wa wanaume, punde baada ya washindi hao kukabidhiwa zawadi zao.
Mratibu wa Mbio za Rock City Marathon 2014 kutoka kampuni ya Capital Plus International Limited (CPI), akizungumza na waandishi wa habari juu ya muitikio mkubwa ulionyeshwa katika Mbio za mwaka huu zilizofanyika Jijini Mwanza Jana.
 Mwanariadha kutoka Mkoani Manyara Joseph Panga,akimaliza mbio za KM 21 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza jana,wakati wa mbio za Rock City Marathon 2014, akifuatiwa na Sammy Nyokaye kutoka Kenya(kulia).
 Wanariadha wakianza kukimbia mbio za km 21 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza jana,wakati wa mbio za Rock City Marathon 2014.


Mbio za Rock City 2014 zatiafora
  • Mtanzania ashinda mbio za kilometa 21
Mwandishi Wetu, Mwanza
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Evarist Ndikilo ameagiza maofisa utamaduni na michezo kuandaa mikakati jinsi ya kushiriki kikamilifu mashindano ya Rock City Marathon mwakani.
Akikabidhi zawadi kwa washindi wa mbio  kwenye uwana wa CCM Kirumba kwa niaba ya Ndikilo jana, Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Amina Masenza alisema licha mbio hizo kufanyika mkoani hapa kwa miaka sita, Mwanza haijafanya vizuri na kuagiza ofisa utamaduni kuandaa mkakati wa kutelekezwa kwa ajili ya mashindano mwakani.
Ndikilo alisema Tanzania inaweza kurejea ramani ya dunia kwenye michezo na kwamba, kinachohitajika ni maandalizi  hasa  kuanzia shule za msingi.

Mashindano hayo yaliyoandaliwa na kampuni ya Capital Plus International (CPI) yamefanikishwa kwa udhamini wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), TSN Group kupitia kinywaji chake cha Chilly Willy, pamoja na African Barrick Gold, IPTL, Air Tanzania, New Mwanza Hotel, Nyanza Bottling, Sahara Media Group, Continental decoders, New Africa Hotel, PPF, Tanapa na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB). 

Naye Rais wa RT, Andrew Mtaka aliagiza waandaji wa mashindano ya riadha nchini kuanza kuwaweka wanariadha kambini kabla ya mashindano, huku akiwataka walimu kutowachosha wanamichezo hao.

Mtaka alisema uhamasishaji wa mbio hizo umekuwa mkubwa na kuwataka waandaji wengine nchini kuiga Kampuni ya Capital Plus, kwani ushiriki wa watoto kwenye mashindano hayo umekuwa mkubwa.

"Waandaaji wote wa mashindano ya riadha wahakikisahe wanazingatia ushiriki wa watoto na watu wenye ulemavu wa ngozi (albino), nitaendelea kulea vijana walioonyesha vipaji ili wawekwe kwenye benki yetu ya wachezaji," alisema Mtaka.

Alisema tayari wameomba Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe ili kuwaisaidia wachezaji kuweka kambi nje ya nchi kama alivyofanya wakati wa michauano ya Jumuiya ya Madola.

Katika mashindano hayo, Joseph Panga kutoka Manyara ameibuka mshindi wa kwanza kwenye mbio za Rock City Marathon zilizofanyika jijini Mwanza jana baada ya kumaliza kwa muda wa saa 1:02:36, akifuatiwa na Mkenya Sammy Nyokaye aliyetumia muda wa saa 1:02:39.

Mbio hizo za kilomita 21 zilizofanyika zilianzia Uwanja wa CCM Kirumba kupitia Barabara ya Uwanja wa Ndege hadi Mzunguko wa Samakisamaki na kurudi hadi Uwanja wa Ndege Mwanza na kumalizikia Kirumba.

Nafasi ya tatu upande wa wanaume ni Festus Talam kutoka Kenya aliyetumia muda wa saa 1:03:05, huku upande wa wanawake Kanda ya Kaskazini ikionekana kutawala mbio hizo, mshindi wa kwanza ni Mathalia Elisante aliyetumia muda wa saa 1:14:25 akifuatiwa na Mary Naali aliyetumia saa 1:15:34 na Adelina Audata saa 1:23:01.

Washindi wa kwanza waliibuka na kitita cha Sh1.5 milioni kila mmoja, washindi wa pili Sh900,000 na washindi watatu Sh700,000.

Akizungumzia siri ya ushindi wake, Panga alisema mashindano ya mwaka jana alishika nafasi ya sita na kwamba, hiyo ilikuwa chachu ya kujituma kufanya zaidi mazoezi na kula vizuri.

"Maandalizi ya mwaka huu ni mazuri ila washiriki ni wachache na hiyo imetokana na wengi wamekwenda kwenye vilabu yao kwa ajili ya mashindano, lengo langu ni kuhakikisha nakimbia Olimpiki ya kimataifa," alisema.

Hata hivyo, Nyokaye alisema mwaka jana alishika nafasi ya nne ingawa washiriki walikuwa wengi tofauti na mwaka huu, huku akishauri Chama cha Ridhaa Tanzania (RT) kujikita zaidi shuleni ambako wanaweza kupata wanariadha wazuri.

Mahindano hayo yanayoandaliwa na Kampuni ya Capital Plus kila mwaka yamo kwenye kalenda ya RT, huu ni mwaka sita tangu kuanzishwa.

Washindi wa kilomita tano wanaume ambazo ni maalumu kwa walemavu wa ngozi (albino) ni Pascal Charles, Pascal Emmanuel wote kutoka Wilaya ya Magu, mkoani Mwanza na George Joseph kutoka Ilemela.

Upande wa wasichana mshindi ni Irene Joseph, Asterina Abel na Saidati Haji wote kutoka wilayani Ilemela, mkoani Mwanza.

Mita 100 washindi wasichana ni Kabula Hamis, Anita Elias na Damari Charles na wanaume ni Erick Charles, Jumanne Roche na Lugera Machumu. Washindi wa mita 400 upande wa wasichana ni Leticia Richard, Pili Hamisi na Paschalia Sylveter.