Wednesday, October 15, 2014

MAONYESHO YA TIBA ASILI KIMATAIFA KUFANYIKA MNAZI MMOJA DAR ES SALAAM KUANZIA ALHAMISI HII



MAONYESHO YA TIBA ASILI KIMATAIFA KUFANYIKA MNAZI MMOJA DAR ES SALAAM KUANZIA ALHAMISI HII
MAONYESHO ya Biashara ya Kimataifa ya Tiba Asili ya Mwafrika yamepangwa kufanyika jijini Dar es Salaam katika Viwanja vya Mnazi Mmoja kuanzia Novemba 16 hadi 23. 

Maonyesho hayo ambayo yanafanyika nchini kwa mara ya kwanza yameandaliwa na Jukwaa la Tiba Asili Tanzania kwa kushirikiana na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na Mamlaka ya ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE). 
Mwenyekiti wa Kamati ya Manndalizi ya Maonyesho hayo, Boniventure Mwalongo alisema jijini Dar es Salaam jana kuwa wadau mbalimbali wa Tiba Asili na Tiba Mbadala wanatarajia kushiriki katika maonyesho hayo.

 Kwa mujibu wa Mwalongo washiriki hao ni pamoja na Watabibu wa Tiba Asili, Watengenezaji wa Dawa Asili, Wakunga wa Tiba Asili, Kampuni za Dawa Asili na vipodozi vya dawa asili, Wasambazaji wa Tiba Asili na Tiba Mbadala, Watengenezaji wa vyakula asili, kliniki za tiba asili na Tiba Mbadala. 

Aidha mwalongo alisema kuwa wanaendelea na taratibu za kufanya maongezi na wadhamini mbalimbalia ambapo watatoa taarifa rasmi baada ya kufikia tamati ya maongezi, ikiwa ni pamoja na kutoa ratiba nzima ya maonyesho hayo. 
"Tunafanya maongezi na wadau mbalimbali ambao wameonyesha nia ya kutusaidia, lakini pia kauli mbiu ya mwaka huu ni 'Ushirikiano wa Tiba Asili na Tiba za kisasa katika kuhimarisha huduma ya Afya Afrika', alisema Mwalongo. 
Aliongezea kuwa hadi sasa wana orodha wadau wasiopungua 280 ambao tayari wameonyesha nia ya kushiriki katika maonyesho hayo, baada ya kuwapelekea taarifa kwa njia mbalimbali za mawasiliano. Kwa mujibu wa Mwalongo, gharama za kushiriki zimegawantika katika makundi tofauti ambapo Watambuzi wa magonjwa, watengenezaji wa dawa asili, wakunga wa tiba asili, Wenye virutubisho vya tiba asili na wauzaji wa dawa asili gharama yao ni 100,000/-. 

Kampuni za dawa asili na vipodozi asili zitalipa 500,000/-. Wasambazaji wa dawa za asili na dawa mbadala watatakiwa kulipa ada ya 1,000,000/-. Wauza vyakula asili watalipia 150,000/- wakati kliniki ya tiba asili watalipia 1,500,000/- Kliniki ya tiba mbadala gharama yake ni 2,000,000/-. Kampuni za virutubisho kutoka nje ya Jumuiya ya Afrika Mashariki zitalipia dola za Marekani 1,500. Viwango vingine ni dola 500 za Marekani kwa Kampuni za Tiba Asili ndani ya Jumuiya ya Afrika Mshariki. 

Gharama za ushiriki kwa Benki, Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na Taasisi za Serikali ni 2,000,000/-. Wajasiliamali wa kazi za uchongaji watalipia 500,000, wakati vyama vya tiba asili vitalipia 1,000,000. Aidha Mwalongo alitoa wito kwa makundi mengine ambayo yangependa kushiriki, kujitokeza mapema ili taratibu ziweze kufuatwa. 
"Huenda kuna makundi mengine ambayo labda tumeyasahau, lakini milango bado iko wazi kwa yeyote ambaye angependa kushiriki maonyesho haya," alisisitiza Mwalongo. 
 Alisema kuwa wana imani baada ya maonyesho hayo kutakuwa na mtandao mkubwa wa kibiashara katika huduma ya tiba asili na tiba mbadala kwa nchi za Afrika na hata nje ya Afrika. Aidha alisema kuwa wako mbioni kuyasajili rasmi maonyesho hayo ili yawe yanafanyika kila Agosti 30 pale inapoadhimishwa siku tiba Asili ya Mwafrika.