Katibu Mkuu Kiongozi Ikulu, Balozi Ombeni Sefue ameeleza kufurahishwa na miradi ya sekta ya afya inayopendekezwa kuingia katika Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN).
Balozi Sefue aliyasema hayo mara baada ya kutembelea jijini Dar es Salaam juzi, maabara inayokutanisha wataalamu mbalimbali kutoka SErikali na sekta binafsi wanaochambua miradi michache ya afya itakayoingizwa katika mfumo wa utekelezaji wa haraka wa miradi wa BRN.
"Binafsi nimefurahishwa na maeneo ya kipaumbele mnayoendelea kuyafanyiakazi ili yapendekezwe kuingia katika BRN. Naahidi kuwa mtakapokamilisha mapendekezo yenu haya Serikali haitasita kuyafanyiakazi," alisema Balozi Sefue.
Balozi Sefue alisisitiza kuwa sekta ya afya ni muhimu katika maisha ya watanzania hivyo kuingizwa kwa baadhi ya miradi yake ya kipaumbele katika BRN kutasaidia kupatikana huduma bora zaidi.
BRN ni mfumo mpya wa utekelezaji wa miradi ya kipaumbele ulioanza kutekelezwa Julai mosi, 2013 ukiwa chini ya Kitengo cha Rais cha Utekelezaji wa Miradi (PDB).
Akizungumza katika kikao hicho, Mtendaji Mkuu wa PDB, Bw. Omari Issa alifafanua kuwa mtindo wa maabara ni moja ya hatua nane katika mfumo wa utekelezaji wa miradi wa BRN ambapo wataalamu mbalimbali hujifungia kwa wiki sita kuchambua sekta husika na kuibua maeneo ya kufanyiwa kazi.
"Katika maabara hii ya afya kama ilivyokuwa katika sekta nyingine zilizoshaingia BRN, wataalamu hawa wamekaa na watafanyakazi hii kwa wiki sita bila kulipwa posho," alisema Bw. Issa na kuwapongeza wataalamu hao kwa kufanyakazi kwa uzalendo.
Maabara hiyo ambayo mpaka sasa imeshakaa kwa wiki tano tayari imebaini maeneo ambayo yatapendekezwa kupewa kipaumbele katika sekta ya afya. Sekta za awali zilizokwishaingia BRN ni elimu, kilimo, maji, uchukuzi, nishati, ukusanyaji mapato na uboreshaji wa mazingira ya biashara.