Tuesday, September 30, 2014

WANAMICHEZO , WANANCHI WAJITOKEZA KUPIMA AFYA BANDA LA NHIF UWANJA WA JAMHURI MOROGORO



WANAMICHEZO , WANANCHI WAJITOKEZA KUPIMA AFYA BANDA LA NHIF UWANJA WA JAMHURI MOROGORO
Na John Nditi, Morogoro

MAMIA ya wanamichezo na wananchi wa Mkoa wa Morogoro, wameendelea kujitokeza kwa wingi katika banda la Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ili kupima afya zao.

NHIF Mkoa wa Morogoro kwa kushirikiana na Makao makuu , wanaendesha zoezi la upimaji wa afya kwa wanamichezo wa Shimiwi sambamba na wananchi wa mkoa huo ikiwa ni sehemu ya majukumu yake ya kutoa huduma kwa wanachama wake na wananchi kwa ujumla.

Zoezi hilo lililoanza Septemba 27, mwaka huu na litaendelea hadi Oktoba 11, mwaka huu siku ya kilele cha mashindano ya 34 ya Shimiwi yanayofanyika mkoani Morogoro ni la bure.

Meneja wa NHIF Mkoa wa Morogoro, Rose Ongara, alisema hayo leo ( Sept 29) wakati akizungumza na mwandishi wa habari hii, kwenye banda la Mfuko huo lililipo ndani ya uwanja wa Jamhuri wa hapa.

Hata hivyo alisema , NHIF ni wadau katika kusaidia michezo ya Shimiwi kwa kujitolea kupima afya za wachezaji kabla ya mchezaji hawajaanza kushiriki kucheza ama baada ya kucheza michezo yao mbalimbali.

Kwa mujibu wa Meneja wa NHIF Mkoa wa Morogoro, kuwa katika zoezi hili , wanamichezo na wananchi wa mkoa huo watapimwa shinikizo la damu (BP), Kisukari,uzito na urefu kwa wahusika na kuainisha uwiano kati ya uzito na urefu na wanaokutwa na matatizo watapewa ushauri wa kilaalamu na madaktari wa Mfuko huo waliopo kwenye banda hilo.

Hivyo alitumia fursa hiyo kuwaomba wanamichezo wa Shimiwi sambamba na wengine pamoja na wakazi wa Morogoro kuutumia muda huyo kwa kujitokeza katika uwanja wa Jamhuri ili kupima afya zao .
Baadhi ya wafanyakazi wa NHIF wakiwajibika kikamilifu kuwahudumia wateja wao ambao ni wanamichezo wa Shimiwi na wananchi wa kawaida ndani ya Uwanja wa Jamhuri wa Morogoro.
Baadhi ya watumishi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) wakiwa kazini ndani ya uwanja wa Jamhuri wa Mjini Morogoro, kwenye mashindano ya Shimiwi 2014 wakiwa tayari kwa uwajibikaji.
Daktari wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya , akimpima mmoja wa wanamichezo wa Shimiwi mwenendo wa msukumo wa damu kabla ya kuanza mashindano .
Daktari wa NHIF akichukua sampuli ya damu ya mteja wake ambaye ni mwanamichezo , wakati wa zoezi la upimaji wa afya.
Mshiriki wa michezo ya Shimiwi 2014 akipima uzito na urefu kwenye banda la NHIF lililopo uwanja wa Jamhuri wa Morogoro.
Wananachi wa Morogoro na wanamichezo wakiwa katika upimaji wa afya zao kwenye banda la NHIF katika uwanja wa Jamhuri Morogoro.