Thursday, September 18, 2014

Tume kujumuika na Wadau kulaani mauaji dhidi ya watu wenye Ualbino



Tume kujumuika na Wadau kulaani mauaji dhidi ya watu wenye Ualbino
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kwa kushirikiana na Chama cha Albino Tanzania (TAS), Under The Same Sun (UTSS) Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu ( SHIVYAWATA), taasisi za kiraia na wadau wengine wameandaa maandamano ya amani sanjari na maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Amani Duniani (International Day of Peace) yatakayofanyika Jumapili Septemba 21,2014 katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.

Kauli Mbiu ya maadhimisho haya ya kitaifa ni "Haki ya Amani kwa wote: Komesha Ukatili na Mauaji Dhidi ya Watu Wenye Ualbino."

Lengo la maadhimosho haya ya amani ni kulaani vikali vitendo vya ukatili na mauaji dhidi ya watu wenye ualbino na kuhamasisha wadau mbalimbali ikiwemo Serikali, jamii, na jumuiya za kimataifa kuchukua hatua kukomesha vitendo hivyo.

Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Jakaya Mrisho Kikwete ambaye atawakilishwa na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii. Wadau mbalimbali wanatarajiwa kushiriki ikiwemo Serikali, asasi za kiraia, taasisi za dini, vyama vya siasa na jumuiya za kimataifa.
Katibu Mtendaji wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Bibi Mary Massay akisisitiza jambo mbele ya waandishi wa habari waliohudhuria mkutano huo uliofanyika leo katika ofisi za Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Mtaa wa Luthuli jijini Dar es Salaam ,Kushoto kwake ni Bibi Ziada Ally Nsembo, Katibu Mkuu wa Chama cha Albino Tanzania.
Bibi Ziada Ally Nsembo( katikati) Katibu Mkuu wa Chama cha Albino Tanzania akiongea na waandishi wa habari, kulia kwake ni Katibu Mtendaji wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Bibi Mary Massay na kushoto kwake ni Afisa kutoka Under The Same Sun (UTSS).
Meneja uendeshaji wa Under The Same Sun (UTSS), Bwana Gamariel Mboya akitoa maelezo mbele ya waandishi wa habari katika mkutano na waandishi hao uliofanyika leo katika Ofisi za Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Mtaa wa Luthuli jijini Dar es Salaam. Kushoto kwake ni Katibu Mtendaji wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Bibi Mary Massay, na Bibi Ziada Ally Nsembo, Katibu Mkuu wa Chama cha Albino Tanzania.
Sehemu ya waandishi wa habari na wadau wengine waliohudhuria mkutano huo.