Thursday, September 18, 2014

SERIKALI, MAKAMPUNI YA MADINI ‘KUWANOA’ WAZAWA KATIKA USHIRIKISHWAJI SEKTA YA MADINI



SERIKALI, MAKAMPUNI YA MADINI 'KUWANOA' WAZAWA KATIKA USHIRIKISHWAJI SEKTA YA MADINI
Kaimu Kamishna wa Madini, Mhandisi Ally Samaje akiwakaribisha wajumbe wa mkutano wa kujadili ushirikishwaji wazawa (local content) katika sekta ya madini uliofanyika jijini Mwanza hivi karibuni. Waliokaa meza kuu kutoka kushoto ni Kamishna Msaidizi Kitengo cha Uchumi na Biashara, Salim Salim, Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza, Ndalo Kulwijila na Mkuu wa Wilaya ya Tarime, John Henjewele.
Mwanasheria wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) Rose Mponguliana akiwasilisha mada kuhusu uwajibikaji wa Shirika hilo katika suala la ushirikishwaji wazawa wakati wa mkutano baina ya Serikali na Makampuni ya Madini uliofanyika hivi karibuni jijini Mwanza.
Wajumbe wa Mkutano baina ya Serikali na Makampuni ya Madini uliojadili  ushirikishwaji wazawa katika sekta ya madini wakisikiliza hotuba ya Mgeni Rasmi, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Ndalo Kulwijila (hayupo pichani).
Wajumbe wa Mkutano baina ya Serikali na Makampuni ya Madini uliojadili  ushirikishwaji wazawa katika sekta ya madini wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya ufunguzi wa mkutano huo katika Hoteli ya Gold Crest jijini Mwanza hivi karibuni. Kutoka Kushoto waliokaa ni Kaimu Kamishna Msaidizi wa Madini Sehemu ya Uongezaji Thamani Madini Latifa Mtoro, Kaimu Kamishna wa Madini, Mhandisi Ally Samaje, Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Ndalo Kulwijila na Mkuu wa Wilaya ya Tarime, John Henjewele.

Na Veronica Simba

Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini pamoja na Makampuni ya Madini nchini, wamekubaliana kuendesha programu za mafunzo kwa wananchi kwa ajili ya kujenga uelewa kuhusu fursa zilizopo katika sekta ya madini ili waweze kuzitumia ipasavyo kuinua vipato vyao na Taifa kwa ujumla.

Makubaliano hayo yalifikiwa na pande hizo mbili hivi karibuni jijini Mwanza wakati wa mkutano ulioandaliwa na Idara ya Madini ya Wizara husika kwa lengo la kuweka mikakati ya pamoja baina yake na Makampuni ya Madini katika kutekeleza Sera ya Madini ya mwaka 2009 inayotoa tamko la sekta hiyo kuwashirikisha Watanzania (local content) na pia kuifungamanisha na sekta nyingine.

Wajumbe wa mkutano huo kwa pamoja walipitisha maazimio kadhaa yaliyolenga kuhakikisha Watanzania wanashirikishwa ipasavyo katika sekta ya madini ambapo mojawapo ya maazimio hayo ilikuwa ni kujenga uelewa kwa wananchi waweze kuzitambua fursa zilizopo na kuzitumia.

Pia, Wajumbe walikubaliana kuwa kufanyike utafiti utakaoainisha mianya iliyopo katika utoaji huduma hususan maeneo ambayo wananchi wanaweza kutoa huduma kwa makampuni ya madini ili huduma zinazoweza kutolewa na wananchi zisitolewe na wageni kutoka nje ya nchi.

Akifafanua kuhusu wananchi kupewa fursa za kutoa huduma kwa makampuni ya madini, Kaimu Kamishna wa Madini, Mhandisi Ally Samaje alisema wananchi wana haki ya kutoa huduma zilizo ndani ya uwezo wao hivyo Serikali itahakikisha haki hiyo inatekelezwa kama inavyostahili.

"Sisi kama Serikali tunataka kuboresha ushirikishwaji wazawa katika sekta ya madini na ni lazima makampuni ya madini yahakikishe wazawa wanashirikishwa ipasavyo," alisisitiza.

Aidha, maazimio mengine yaliyofikiwa katika mkutano huo ni pamoja na Serikali kwa kushirikiana na makampuni ya madini kuwajengea uwezo wazawa (kifedha na utaalamu) kwa kutilia mkazo sekta ya kilimo na uzalishaji.

Vilevile, pande hizo mbili zilikubaliana kwamba, kwa kuwa ushirikishwaji wazawa ni suala la kisera, iko haja ya kufanyia marekebisho sheria na kanuni za madini kuhusu ushirikishwaji wa wazawa ili kuhakikisha wazawa   wanapata haki stahiki.

Pia, iliafikiwa kuwa kuanzishwe kamati maalumu itakayoshughulikia masuala ya ushirikishwaji wazawa katika sekta ya madini ambayo pamoja na mambo mengine itaainisha mahitaji na viwango katika eneo husika katika hali ambayo ni shirikishi, na pia kusaidia kuainisha fursa zilizopo katika sekta.

Wajumbe wa mkutano huo pia walikubaliana kuwa Wizara ya Nishati na Madini iandae mkutano wa kila mwaka kujadili suala la ushirikishwaji wazawa ambao utashirikisha makampuni yote ya madini, wafanyabiashara   na wazalishaji wazawa, jamii zinazozunguka migodi pamoja na wizara na taasisi nyingine za serikali zinazohusika.