Friday, August 29, 2014

WAZIRI MKUU ATUMA SALAMU ZA RAMBIRAMBI IRELAND



WAZIRI MKUU ATUMA SALAMU ZA RAMBIRAMBI IRELAND
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda ametumua salamu za rambirambi kwa Serikali ya Ireland kufuatia kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu wa zamani wa nchi hiyo, Bw. Albert Reynolds.

Hayati Reynolds ambaye amefariki akiwa na miaka 81, alikuwa Waziri Mkuu wa nane wa nchi hiyo kwa miaka mitatu kuanzia mwaka 1992. Atakumbukwa kwa kuanzisha mchakato wa kuleta amani Ireland Kaskazini dhidi ya kundi la IRA.

Waziri Mkuu Pinda ambaye aliwasili jana (Alhamisi, Agosti 28, 2014) jijini Dar es Salaam akitokea Dodoma, alikwenda moja kwa moja ubalozi wa Ireland na kusaini kitabu cha maombolezo cha kiongozi huyo.

Katika salamu za rambirambi, Waziri Mkuu amemwelezea Bw. Reynolds kuwa ni kiongozi atakayekumbukwa kwa kuleta amani duniani na misaada ya kimaendeleo nchini Tanzania. 

"Kwa niaba ya Serikali ya Tanzania, ninawapa pole sana kwa kufiwa na Kaka yetu na ndugu yetu, Waziri Mkuu wa zamani wa Ireland, Albert Reynolds. Tunashirikiana nanyi katika kipindi hiki cha majonzi. Tutaendelea kumkumbuka kwa kazi nzuri alizofanya kwa nchi yetu na duniani. POLENI SANA KWA MSIBA HUU MKUBWA," inasomeka sehemu ya salamu za rambirambi alizotoa Waziri Mkuu.

Akipokea salamu hizo, Balozi wa Ireland nchini Tanzania, Bibi Fionnuala Gilsenan alimshukuru Waziri Mkuu Pinda kwa kufika ubalozini hapo na kuwapa pole kwa kifo cha Waziri Mkuu wao wa zamani. 

"Tutamkumbuka kiongozi wetu kwa mambo mengi aliyoifanyia nchi yetu… Tunafarijika kwa salamu hizi za rambirambi. Tutafikisha kitabu hiki cha salamu za rambirambi kwa familia yake, naamini nao watafarijika sana," alisema Balozi Gilsenan.

Balozi Gilsenan alimweleza Waziri Mkuu kwamba kitabu cha maombolezo kitafungwa leo.