Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Mazingira Suzi Salula akifafanua jambo kwa waandishi wa habari kuhusu mabadiliko ya tabianchi leo jijini Dar es Salaam ambapo Tanzania inatarajiwa kuwa mwenyeji wa mkutano wa Mawaziri wa Mazingira na Mambo ya nje kutoka nchi za kamati ya wakuu wa Nchi za Afrika unatarajiwa kufanyika Agosti 29, 2014 nchini.
Waziri wa Nchi , Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira Dkt Binilith akizunguza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam kuhusu mkutano wa Mawaziri wa Mazingira na Mambo ya nje kutoka nchi za kamati ya wakuu wa Nchi za Afrika unatarajiwa kufanyika Agosti 29, 2014 nchini.
-----
Na Lorietha Laurence.
Waziri wa Nchi , Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira Dkt. Binilith Mahenge ametoa wito kwa wananchi kuunga mkono juhudi za serikali na za Bara la Afrika kupambana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi ili kupata maendeleo endelevu.
Hayo yalisemwa jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mkutano wa Mawaziri wa Mazingira na Mambo ya nje kutoka nchi za kamati ya wakuu wa Nchi za Afrika unatarajiwa kufanyika Agosti 29, 2014.
Mkutano huu wenye lengo la kujadili na kupendekeza masuala muhimu ya bara la Afrika kuhusu upatikanaji wa fedha na teknolojia katika kukachangamoto hizo zinazo athiri sekta ya kilimo, usafirishaji, afya, nishati,mifugo,uvuvi,viwanda na maji.
"ni jukumu letu sote kuhakikisha tunakabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi kwa kutumia gesi na majiko maalum ili kupunguza gesijoto inayopelekea mabadiliko ya tabia ya nchi" alisema Dkt. Mahenge
Aidha aliongeza kuwa mkutano huo ni maandalizi ya mkutano unaotarajiwa kufanyika Septembe 23, 2014 ulioitishwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na ule wa 20 wa Nchi wananchama wa Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi utakaofanyika Mjini Lima, nchini Peru Desemba 1-12,2014.
Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Mazingira Suzi Salula aliongezea kuwa juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi zinahitajika kutiliwa mkazo ili kuweza kujikwamua kuondokana na changamoto hii.
Ripoti ya Wataalamu wa Kimataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi inaonyesha kuwa mwaka 2013 joto la dunia limeongezeka kwa nyuzi joto 0.85 juu ya wastani wa joto la dunia na kupelekea ongezeko la gesijoto na kuathiri kwa kiasi kikubwa sekta ya Kilimo, nishati, afya, usafirishaji, mifugo, uvuvi, viwanda na maji.