MACHESTER United ikicheza soka la hali ya juu, imeendeleza wimbi la ushindi katika mechi zake za kupasha moto baada ya kuitandika Valencia ya Hispania bao 2-1.
Shujaa asiyetarajiwa katika mchezo huo akawa ni Marouane Fellaini aliyeifungia United bao la ushindi katika dakika za majeruhi na kuifanya timu hiyo iwe imeshinda mechi zake zote (sita) za majaribio.
Fellaini aliyeingia dakika ya 76 kuchukua nafasi ya Hernandez akapata wasaa wa kucheza kwenye nafasi yake aliyoizoea (kiungo) na kulishika ipasavyo dimba la kati.
Nyota huyo wa Ubelgiji alizunguka huko na kule akikota na kusambaza mipira kwa pasi za uhakika huku akionyesha pia uwezo mkuwa wa kubadilisha mwelekeo wa mchezo
Bao la kwanza la United lilifungwa na Fletcher katika dakika ya 49 hii ikiwa ni baada ya Rooney kukosa penalti kipindi cha kwanza.
Valencia walisawazisha ilipotimu dakika ya 57 kupitia kwa Rodrigo kabla ya Fellaini kuipatia ushindi United dakika ya 90+1.
Fellaini ambaye ndiyo alikuwa anacheza mchezo wake wa kwanza msimu huu, alipokea pasi ndefu ya beki kinda Blackett na kuutuliza mpira kifuani mbele ya kipa Alves kabla ya kuujaza wavuni kwa guu lake la kushoto.
Huu unakuwa mchezo wa kwanza wa majaribo wa Manchester United kwenye uwanja wake wa nyumbani (Old Trafford).
Van Gaal amabaye aliingia Old Trafford kwa mara ya kwanza kama kocha wa United na kupokewa kwa shangwe kubwa, alionyesha uso uliojaa matumani pasi na shaka yoyote ya kuifanyia makubwa timu hiyo.
Manchester United: De Gea; Jones, Smalling (M.Keane 62), Blackett; Young (Lingard 62), Fletcher (Cleverley 62), Herrera (Januzaj 76), Mata (Kagawa 62), James; Rooney, Hernandez (Fellaini 76).
Valencia: Alves; Barragan, Otamendi, Gaya, Vezo; Fuego, Feghouli (Rodrigo 57), Parejo, Moreno (Araujo 90), Gomez (Guardado 73); Alcacer (Piatti 57).