Tuesday, August 19, 2014

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar akutana na Balozi wa Uholanzi Nchini Tanzania



Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar akutana na Balozi wa Uholanzi Nchini Tanzania
Serikali ya Uholanzi inakusudia kuongeza fursa zaidi za masomo kwa wanafunzi wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania katika kupata taaluma ya juu kwenye vyuo vikuu mbali mbali nchini humo.

Kauli hiyo imetolewa na Balozi wa Uholanzi Nchini Tanzania Bwana Jaap Frederiks wakati akibadilishana mawazo mbali mbali na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo Ofisini kwake Mtaa wa Vuga Mjini Zanzibar.

Balozi Jaap Frederiks alisema wapo wanafunzi wengi wa Kitanzania wanaohitaji kupata elimu ya juu baada ya kumaliza masomo yao ya sekondari lakini kinachowakwaza ni ufinyu wa kupata fursa kama hizo unaosababishwa na ukosefu wa ufadhili.

Balozi huyo wa Uholanzi aliishauri Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuangalia sekta na maeneo ambayo Nchi yake inaweza kusaidia kitaaluma na hata uwezeshaji.

Bwana Jaap alifahamisha kwamba zipo fursa nyingi katika sekta ya elimu, mazingira, kilimo, ufugaji na hata mawasiliano nchini uholanzi ambazo kama kutakuwa na utaratibu muwafaka zinaweza kuifaidisha Zanzibar kiuchumi na ustawi wa jamii.

Naye Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliipongeza Uholanzi kupitia Balozi Wake huyo kwa jitihada inazochukuwa nchi hiyo katika kusaidia maendeleo ya Tanzania na Zanzibar kwa ujumla na kutoa wito kwa wawekezaji na watalii wa Nchi hiyo kuendelea kutumia fursa iliyotolewa na Zanzibar katika uimarishaji wa sekta ya utalii na uwekezaji vitega uchumi.
Balozi wa Uholanzi { Netherland } Nchini Tanzania Bwana Jaap Frederiks akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Ofisini kwa Makamu Vuga Mjini Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akibadilishana mawazo na Balozi wa Uholanzi Nchini Tanzania Bwana Jaap Frederiks aliyepo kati kati Ofisini kwake Vuga. Pembeni yao aliyepo kushoto ni Ofisa wa ubalozi huo Bwana Dick Jan Brower.
Balozi wa Uholanzi Nchini Tanzania Bwana Jaap Frederiks akiagana na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif mara baada ya mazungumzo yao yaliyofanyika ofisini kwa Makamu wa Pili Vuga Mjini Zanzibar. Picha na Haasn Issa wa –OMPR – ZNZ.