Thursday, August 14, 2014

Katiba itakuwa ni ya Makundi yote - Mh. Sitta




Katiba itakuwa ni ya Makundi yote - Mh. Sitta
Na Magreth   Kinabo

Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Mhe. Samuel Sitta amewahakikkishia Watanzania kwamba  Katiba Mpya itakayopatikana itakuwa imezingatia matakwa ya makundi mbalimbali.

Mhe . Sitta aliyataja makundi hayo  baadhi ya  makundi hayo kuwa ni wafugaji, wakulima, wavuvi na wasanii.Huku akisema Katiba Mpya itakayopatikana itakuwa ni bora kuliko ya iliyopo sasa.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Mhe . Sitta wakati akizungumza na wafugaji wapato 44 kutoka mikoa mbalimbali,ambao waliongozwa na Mwenyekiti wa ujumbe huo, Huruma Ole Kalaita na Mlezi wao, ambaye mjumbe wa Bunge hilo na Mbunge wa Jimbo la Maswa Magharibi(CHADEMA).

"Tunaamini ni wakati wa Katiba Mpya… lazima iweze kupatikana. Itakayozingatia Sheria bora na maslahi ya makundi mbalimbali  yatapatikana.

" Utungaji wa Katiba ni suala la wananchi kutanguliza suala la muundo wa Serikali si haki. Ni muhimu kutanguliza haki za raia. Kinachotangulia ni haki za raia wetu na makundi mbalimbali," alisisitiza Mhe. Sitta.

Aidha Mhe. Sitta aliwakikishia wafugaji hao,kwamba Bunge hilo " liko hapa kisheria kwa kanuni zake linaendelea na wale wanaopiga kelele hawalitakii mema taifa letu kwa sababu demokrasia  yoyote ni kupata kura ya walio wengiu," alisema.   

 Kwa upande wake Mlezi wa wafugaji hao, Mhe. Shibuda alimpongeza Mhe. Sitta kwa jitihada zake za kuendeleza  vikao vya Bunge hilo, ambapo pia alimsihii kuwa asikatishwe tamaa kwa dhamira yake njema ya  kuendelea kuongoza vikao vya  Bunge hilo.

Akizungumzia kuhusu masuala ya wafugaji hao na wakulima wa zao la pamba nchini, alisema kuwa wako pamoja  naye.

" Hivi Serikali tatu au mbili inatiririsha nini kwa wakulima na wafugaji. Tunataka viongozi wa kukabiliana na matatizo ya  wananchi," alisisitiza Shibuda.

Kwa upande  Mwenyekiti wa wafugaji hao, Kalaita alipendekeza Katiba Mpya, itamke matumizi bora ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji ili kuondoa migogoro ya wakulima na wafugaji.

 Makamu wa Mwenyekiti wa wafugaji hao, Kasundwa Wamalwa kutoka Kanda ya Magharibi akisoma mapaendekezo ya risala yao waliyoiwasilisha kwa Mwenyekiti wa Bunge hilo, Mhe. Sitta, ambapo walipendekeza Katiba Mpya itambue wafugaji wa asili.

 Aidha Makamu Mwenyekiti huyo aliwataka wajumbe wa Bunge hilo, kuwa na hofu ya  Mwenyezi Mungu wakati wanapoendelea na mchakato huo.

Miongoni mwa makundi mengine waliofika katika ofisi za Bunge mjini Dodoma ni Jukwaa la Katiba (JUWAKATA) na Jukwaa la Wahariri.