Thursday, August 14, 2014

DAWASCO YAPATA BODI MPYA



DAWASCO YAPATA BODI MPYA
Na Athumani Shariff (MoW)
Waziri wa Maji Prof. Jumanne Maghembe, leo amezindua rasmi BODI mpya ya Shirika la majisafi na Usafi wa Mazingira (DAWASCO) inayoundwa na wajumbe 13. BODI hii  imeundwa baada ya ile ya zamani kumaliza muda wake.
Bodi hiyo mpya imeteuliwa tangu tarehe 1/8/2014 inayojumuisha wataalam mbalimbali wakiwemo maprofesa wa chuo kikuu cha Dar es Salaam, viongozi wa kisiasa na asasi za kiraia inaongozwa na Mwenyekiti Meja Generali Mstaafu Samweli Kitundu.
Pia wamo Nehemia Mchechu, Mkurugenzi Mtendaji Shirika la Nyumba la Taifa, Prof. Samweli Maghimbi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dkt. Marcelina Chijiriga Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Teresia Mbando katibu Tawala Ofisi ya Mku wa Mkoa wa Dar es Salaam, Hawa Sinare Mwenyekiti wa BODI ya DAWASA.
Wengine ni Inj. Ray Seng'enge, Abubakari Kunenge, Inj. Boniface Muhegi, Iddi Azan Zungu, Blangson Hamisi na Katibu wao Jackson Midala Mkurugenzi wa Shirika la Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASCO).
Profesa Maghembe aliitaka BODI hiyo kuzikabili vilivyo changamoto zote zinazolikabili shirika hilo, hususan upotevu wa maji ambao umefikia asilimia 55 sasa.
"Naagiza muunde mara moja kitengo cha ki-intelijensia zaidi kitakachoripoti mara moja kwenye bodi yenu juu ya wizi wa maji" Aliagiza Waziri Maghembe.
Waziri alisema, hivi karibuni tunategemea kupata maji mengi sana kwa ajili ya jiji la Dar es Salaam, hivyo yatakuwa hayana umuhimu endapo yakuwa yanapotea wakati serikali imeekeza pesa nyingi sana katika kuyaleta. Alieleza Waziri Maghembe.
Pia aliitaka BODI iandae mpango wa kulipa madeni yanayodaiwa haswa na shirika la umeme Tanzania (TANESCO) ili kuepuka kusitishiwa huduma hiyo.
Katika hatua nyingine Waziri Maghembe aliitaka BODI hiyo ifanye marekebisho ya menejimenti ili kuleta ufanisi zaidi wa kazi.

Mwisho aliwaambia wafanye kazi kwa bidii wakizingatia matokeo, na aliwaambia kuwa Wizara ya Maji inatekeleza mipango yake kwa haraka kwa utaratibu wa TEKELEZA SASA KWA MATOKEO MAKUBWA yaani BIG RESULTS NOW hivyo ni lazima wajiunge na familia ya maji kwa kufanya kazi kwa utaratibu huo.