Monday, July 07, 2014

TANZANIA YAPIGA HATUA KATIKA UDHIBITI WA SILAHA NDOGO NDOGO NA NYEPESI



TANZANIA YAPIGA HATUA KATIKA UDHIBITI WA SILAHA NDOGO NDOGO NA NYEPESI
Na Frank Geofray-Jeshi la Polisi. 

 Imeelezwa kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa katika kukabiliana na tatizo la uzagaaji wa silaha ndogo ndogo na nyepesi kutokana na nchi nyingine za Afrika kuja kujifunza jinsi ya kukabiliana na tatizo hilo hapa nchini. 

 Hayo yalisemwa na Mkurugenzi wa maendeleo ya Jinsia kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto Bw.Meshack Ndaskoi wakati akifungua semina ya jinsia na uthibiti wa silaha ndogondogo na nyepesi iliyofanyika katika chuo cha Taaluma za Polisi (DPA) jijini Dar Es Salaam jana na kuwashirikisha wadau wa usalama na jinsia hapa nchini. 
 Bw. Ndaskoi alisema Tanzania imekuwa ikifanya vyema kutokana na kuchukua hatua mathubuti ikiwemo ya kuziweka alama silaha zote zilizopo nchini ili kuweza kutambulika kwa urahisi pindi zinapotumika katika matukio ya uhalifu. 
 "Tumeweza kutekeleza sera ya kudhibiti silaha na kuunda kamati ya kitaifa ya kudhibiti uzagaaji wa silaha ndogondogo na nyepesi hapa nchini na yamekuwa yakitolewa mafunzo mbalimbali kwa wadau ili kuungana katika kulikabili tatizo hili" Alisema Ndaskoi. 
 Kwa upande wake Mratibu wa kitaifa wa Kudhibiti silaha ndogondogo na nyepesi Nchini, Kamishna Msaidizi wa Polisi Essaka Mugasa amesema lengo la Semina hiyo ni kutathmini kwa kina mahusiano yaliyopo baina ya uzagaaji wa silaha na jinsia hapa nchini na barani Afrika kwa ujumla kwa kuwa tatizo hilo hivi sasa limekuwa likikua siku hadi siku. 
 Aidha alisema pamoja na zoezi la kuweka alama silaha ambalo linaendelea hivi sasa lakini pia wanafanya operesheni za mara kwa mara na kutumia dhana ya Polisi Jamii na ulinzi shirikishi katika kupata taarifa kutoka kwa raia wema.
Alisema kwakupitia Polisi Jamii na ulinzi shirikishi wamekuwa wakipata taarifa ambazo zimewezesha kusalimishwa kwa silaha mbalimbali hapa nchini ambazo zilikuwa zikimilikiwa isivyo halalai. 
Nao washiriki wa Semina hiyo walisema itawasaidia katika utendaji kazi wao wa kila siku na kutoa elimu kwa wengine ili kutokomeza uzagaaji wa silaha ndogondogo na nyepesi hapa nchini.