Mkuu wa mkoa wa Mtwara Mhe Joseph Simbakalia akimkaribisha Waziri wa Nishati na Madini pamoja na ujumbe alioambatana nao akiwemo balozi wa China nchini Bw…. Mara baada ya kufika ofisini kwake kuelezea uwepo wapo katika mkoa huo
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe John Simbakalia akimweleza Waziri wa Nishati na Madini jambo linalohusu sekta ya umeme ambapo Prof. Muhongo anaisimamia ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Mkandarasi anayehusika na usambazaji wa umeme vijijini Bwana Luta (mwenye shati nyeupe), mara baada ya kusimamishwa na Waziri wa Nishati na Madini Prof Muhongo ili kuelezea maendeleo aliyoyafikia katika kukamilisha mradi huo kulia kwake ni Mkurugenziwa Huduma za Ufundi (REA) Injinia Bengiel H. Msofe.
Prof Muhongo na balozi wa China wakikgua mtambo wa kuchujia maji uliopo katika maeneo ya makazi ya watumishi ambao utawasaidia wananchi wanaozunguka eneo hilo kupata huduma ya maji safi na salama.
Waziri wa Nishati na Madini na ujumbe wake wakikagua mradi wa ujenzi wa nyumba za kuishi watumishi wa mtambo wa kufua gesi lililopo katika eneo la Madimba Mkoani Mtwara
Baadhi ya nyumba zitakazotumika kwa kuishi watumishi wa eneo la kuchakata gesi Madimba ni nyumba za kisasa zilizojegwa kwa ubora mkubwa sana kama zinavyoonekana.
--------------------------
Waziri wa Nishati na Madini Prof Sospeter Muhongo akiambatana na Balozi wa China nchini Dk. Lu Youging wamefanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa bomba la gesi linalotarajiwa kuleta mabadiliko makubwa ya kiuchumi kwa watanzania na hivyo kuchangia kuiingiza nchi kati ya nchi zenye uchumi wa kati ifikapo 2025.
Akizungumza na waandishi wa habari balozi alisema ziara za kukagua bomba la gesi zinalenga katika kuhakikisha kazi inayofanyika ni bora na ipo katika viwango vinavyotakiwa na kuifanya nchi yake kuwa sehemu ya mradi na maendeleo ya nchi.
Kwa upande wake Prof. Muhongo amefurahishwa na maendeleo ya ujenzi wa mradi huo na kukiri kuwa kila mara afanyapo ziara kwenye miradi hiyo anakuta mabadiliko makubwa yanayomfanya kufurahia juhudi ya wakandarasi itakayopelekea mradi kukamilika kwa wakati uliopagwa mezi desemba 2014.
"Jamani ni nani walikuwepo tulipokuwa tukikabidhiwa eneo hili kwa ajili ya kuanza mradi? Eneo hili lilijaa mikorosho tu, lakini sasa tunaona kazi kubwa ya ujenzi iliyofanywa na wakandarasi hawa.
Aidha Muhongo alipotakiwa kueleza manufaa watakayoyapata wananchi wa Lindi na Mtwara alishangaa kuona kuwa bado watu hawaoni manufaa hayo na kuwaeleza waandishi wa habari kutosubiri yeye ndio aseme wakati wao wenyewe wanashuhudia wananchi wakipata ajira, huduma za jamii zikiboreka, wakipewa kipaumbele katika masuala ya elimu.
Hata hivyo Muhongo amewaeleza wanamtwara kuwa wasitegemee manufaa ya kuwepo kwa rasilimali ya gesi ni kuwagawia pesa aidha wanatakiwa kujiendeleza kielimu na kutumia fursa zinazojitokeza ikiwa ni pamoja na ufadhili wa masomo vilivyo ili waweze kujikwamua kimaisha na kushiriki katika kunufaika na gesi iliyogunduliwa katika eneo lao.
Akizungumzia suala la kukamilika kwa mradi huo msimamizi wa ujenzi wa bomba hilo Injinia Balthazar Mrosso alisema limekamilika kwa asilimia 70 na maeneo yaliyosalia ni yale yanayohitaji umakini mkubwa ikiwa ni pamoja na maeneo yanayoathiriwa na mafuriko pembezoni mwa mto wa Ruvu ambako kazi ya kuchimba mashimo ili kufukia mabomba hayo inaendelea, maeneo yenye miinuko na madaraja.
Akielezea suala la kukamilika kwa miradi ya kusambaza umeme vijijini Prof. Muhongo amesema miradi yote nchini inatakiwa kukamilika ifikapo juni 2015 na kuagiza mkandarasi asiye na uwezo wa kufanya hivyo kurudisha mradi huo apewe mtu mwenye uwezo.
Muhongo alimtaka mkandarasi Luta kuelezea hatua aliyofikia katika kusambaza umeme huo katika mkoa wa Mtwara ambapo alieleza kuwa suala la kusafisha mkuza limekamilika pamoja na kusambazwa na kusimikwa kwa nguzo kwa eneo Fulani. Aidha Mkandarasi Luta alimhakikishia Profesa Muhongo kuwa mradi huo utakamilika kwa wakati.
Akitanabaisha nia ya dhati ya kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati Muhongo alisema kuanzia mwezi huu hadi mwezi Oktoba atakagua miradi yote ya REA II na kwa wakandarasi watakaoonesha kutoridhisha kupokonywa miradi. "Hatutasubiri kufika mwezi juni ndipo tuanze kufukuzana na kukamilika kwa miradi mpaka desemba wakandarasi watakaoonesha kuzubaa watapokonywa na kupewa mtu mwingine awe mzawa au mgeni" alisisitiza Muhongo.
Tangia kuanza kutekelezwa kwa mradi huo mkubwa wa Bomba la gesi hii ni mara ya tatu kwa profesa Muhongo kuzungukia maeneo hayo kujionea jinsi kazi inavyofanyika na kukiri kufurahishwa na kasi ya wakandarasi hao.