IKIWA zimabakia siku chache kuanza kwa shughuli za maonesho ya sikukuu za wakulima nane nane zinazotarajia kuanza Agosti Mosi Mwaka huu kanda ya Nyanda za juu kusini lakini bado maandalizi yake yanasuasua. Maonesha hayo ambayo hufanyika kila mwaka katika viwanja vya John Mwakangale Uyole jijini Mbeya huandaliwa na Chama cha Wakulima Tanzania (TASO). Akizungumzia maandalizi ya mwaka huu, Katibu wa TASO kanda ya Nyanda za juu kusini, Ramadhani Kiboko, alikiri kusuasua kwa maandalizi ya sikukuu za wakulima nanenane mwaka huu tofauti na miaka iliyopita. Kiboko alisema kawaida kila mwaka maandalizi na shamla shamla za washiriki kuanza kuandaa maeneo yao pamoja na vipando huanza Juni 30 lakini hadi sasa hakuna kinachofanyika pamoja na jitihada za kuanza kutumika kwa stendi mpya. Alisema tangu mwezi Machi mwaka huu TASO ilitoa barua za mialiko ya kushiriki maonesho ya mwaka huu kwa washiriki 399 ambao ni pamoja na Halmashauri za Kanda, Taasisi za Serikali, bodi za mazao, Taasisi za majeshi,Wizara za Serikali na vituo vya utafiti. Alisema lakini katika watu wote hao walioalikwa ni washiriki 298 waliothibitisha kushiriki kwa maandishi na wengine kwa kukarabati maeneo watakayoyatumia pamoja na kuboresha vipando vyao. Aidha Katibu alitoa wito kwa waalikwa wengine ambao bado hawajajibu kama watashiriki kufanya hivyo mapema na kuanza kufanya maandalizi tayari kwa maonesho yatakayoanza Agosti Mosi Mwaka huu. Aliongeza kuwa kuna wengine ni wageni hawajawahi kushiriki maonesho hivyo ni nafasi yao kuwahi ili waweze kuoneshwa maeneo na kuanza maandalizi ya vitu wanavyotarajia kuvifanya wakati wa sherehe hizo. Pia alitoa wito kwa wafanyabiashara mbali mbali kutumia Uwanja wa John Mwakangale katika biashara zao kwa kuendeshea magulio au minada ya bidhaa mbali mbali kipindi ambacho kunakuwa hakuna maonesho. Mwisho. Na Mbeya yetu |