HADI dakika ya 29 tayari Ujerumani walishamaliza mpira. Walikuwa wanaongoza 5-0 dhidi ya wenyeji wa FIFA World Cup 2014 – Brazil. Hakukuwa na miujiza ya Brazil 'kufufuka' na kurejea mchezoni.
Ni katika mchezo wa nusu fainaili ulioshuhudia kila 'muvu' ya Ujerumani ikizaa goli, ni kama vile Brazil walikuwa wefungwa mawe miguuni.
Magoli ya Thomas Mueller dakika ya 11, mkongwe Miroslav Klose - ambaye anakuwa mchezaji wa kwanza kucheza kwenye nusu fainali nne za kombe la dunia - dakika ya 23, Toni Kroos aliyefunga mabao mawili dakika ya 24 na 26 pamoja na Sami Khedira aliyetupia wavuni bao la tano kunako dakika ya 29, yalitosha kutoa picha mambo matatu kwa wenyeji: Aibu, fedheha na matusi.
Kocha wa Brazil Luiz Felipe Scolari alikuwa na kazi moja tu: kushika kichwa chake na kujiachia kama mzigo kwenye benchi la akiba kila bao la Ujerumani lilipotinga wavuni.
Kilichobakia baada ya hapo ni Ujerumani kucheza kama vile wako mazoezini, wakionyesha kujiamini na kutibua mipango yote ya Brazil ambao kwa hakika walicheza soka la kawaida kama si bovu.
Maskini! Brazil inapoteza kwa aibu rekodi yake bab kubwa ya kutofungwa nyumbani katika mechi ya kimashindano kwa miaka 39 mfululizo.
Pengine katika dakika ya 32 tungeweza kushuhudia bao la sita pale Toni Kross alipodondosha krosi ndani ya box la Brazil ambapo Fernandinho aliupangua mpira kwa mkono lakini mwamuzi Marco Rodriguez wa Mexico badala ya kuashiria penalti akaamuru mpira uwe kona.
Brazil ambao huko miaka ya nyuma walipenya kwenda fainali katika nusu fainali zao sita za mwisho, sasa watalazimika kugombea nafasi ya tatu na moja kati ya Argentina au Holland.
Kwa Miroslav Klose kufunga kwenye mchezo huu, anavunja rekodi ya mabao 15 ya Ronaldo de Lima na sasa mkongwe huyo mwenye umri wa miaka 36 anayekipiga katika timu ya Lazio ya Italia, anakuwa ndiye mchezaji mwenye magoli mengi zaidi kwenye kombe la dunia kuliko yeyote yule.
Hii inakuwa ni kisasi kizuri kwa Klose aliyekuwepo kwenye kikosi cha Ujerumani kilichofungwa na Brazil ya Ronaldo katika mechi ya fainali ya kombe la dunia mwaka 2002.
Kabla ya mechi hii, mara ya mwisho Brazil kufungwa mabao 5 kwenye kombe la dunia ilikuwa ni mwaka 1938 dhidi ya Poland.
Brazil waliojitutumua kipindi cha pili baada ya kuwaingiza Paulinho na Ramires kuchukua nafasi za Hulk na Fernandinho walijikuta wanapachikwa bao la sita dakika 69 kupitia kwa mshambuliaji wa Chelsea Andre Schuerrle.
Lakini kama vile hiyo haikutosha, dakika kumi baadae Andre Schuerrle aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Klose, akatupia wavuni bao la saba na kuzidi kufanya nyuso za mashabiki wa Brazil waliojazana uwanjani ziendelee kuunda maporomoko ya machozi.
Ozil akakosa bao la wazi dakika ya 89 kabla ya Oscar kuifungia Brazil bao la kufutia machozi dakika moja baadae.
Mara ya mwisho timu kushinda angalau kwa magoli matano kwenye nusu fainali za kombe la dunia ni Juni 24, 1958 pale Brazil ilipoichapa Ufaransa 5-2.
Brazil: Julio Cesar, Maicon, Dante, Luiz, Marcelo, Gustavo, Fernandinho (Paulinho 46), Hulk (Ramires 46), Oscar, Bernard, Fred (Willian 69). Subs: Jefferson, Dani Alves, Maxwell, Henrique, Hernanes, Willian, Jo, Victor.
Germany: Neuer, Lahm, Boateng, Hummels (Mertesacker 46), Howedes, Schweinsteiger, Khedira (Draxler 76), Muller, Kroos, Ozil, Klose (Schurrle 58). Subs: Zieler, .
Running riot: Germany scored four goals in six first-half minutes during Tuesday's semi-final against Brazil