Friday, June 06, 2014

WAMPIGISHA KWATA WAZIRI WA AFYA



WAMPIGISHA KWATA WAZIRI WA AFYA
Wabunge wanawake bila kujali itikadi za vyama juzi usiku waliungana kuibana Serikali wakishinikiza iongeze fedha za Bajeti ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ya mwaka 2014/15 ili kukabiliana na vifo vya kina mama na watoto.

Kibano hicho kilianza mapema asubuhi lakini moto zaidi uliwaka jioni wakati Bunge lilipokaa kama kamati kupitisha bajeti hiyo iliyotengewa Sh622 bilioni, ikiwa ni pungufu ya Sh131 bilioni ya bajeti ya wizara hiyo mwaka 2013/14 ambayo ilitengewa Sh753 bilioni. Wabunge wanawake 10 na wanaume wawili walichangia ikiwamo kutoa shilingi.(Martha Magessa)
Kambi ya Upinzani ilianza kuibana Serikali ikisema imeweka rehani wananchi wake kutokana na kitendo chake cha kuchangia kiasi kidogo cha fedha za maendeleo za wizara hiyo.
Akiwasilisha taarifa ya kambi, Waziri Kivuli wa Afya, Dk Anthony Mbassa alisema Bajeti ya Sh622 bilioni na fedha za maendeleo ni Sh305 bilioni ambazo kati ya hizo, Serikali itatoa Sh54 bilioni tu, wakati washirika wa maendeleo watatoa Sh251 bilioni.
"Hii inaonyesha wazi kuwa Serikali imeendelea kuweka rehani wananchi wake kutokana na bajeti kuendelea kuwa tegemezi kwa wahisani," alisema.
Kibano cha wanawake
Licha ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu wa Bunge), William Lukuvi, Waziri wa Afya, Dk Seif Rashid na Naibu Mawaziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba na Adam Malima kutoa ufafanuzi, walishindwa kuwashawishi wabunge hao waliokuwa wakililia nyongeza ya bajeti.
Hoja hiyo, iliibuliwa na Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Cecilia Paresso baada ya kuondoa shilingi akiitaka Serikali itoe majibu ya sababu za kutoa Sh387 bilioni pekee kati ya Sh753 bilioni za bajeti ya mwaka 2013/14, jambo ambalo limekwamisha utendaji kazi wa wizara hiyo, ikiwa ni pamoja ya kushindwa kutekeleza Azimio la Abuja kuwa kila nchi itenge asilimia 15 ya bajeti kuu kwa ajili ya Wizara ya Afya ili kunusuru vifo vya kina mama na watoto.
Baada ya kauli hiyo wabunge kadhaa walisimama na kuunga mkono hoja hiyo licha ya Mwigulu kulieleza Bunge kuwa Serikali imepanga kuongeza kiasi cha fedha kilichobaki kabla ya Juni 31, mwaka huu.
Hoja hiyo ilifafanuliwa na Malima ambaye alisema Serikali imetoa Sh12 bilioni na kwamba tayari fedha hizo zimeshaingizwa katika akaunti ya Wizara ya Fedha kwa ajili ya kulipia deni la Bohari Kuu ya Dawa (MSD), ambalo ni Sh89 bilioni na deni la matibabu nje ya nchi ambalo ni Sh21 bilioni.
"Kwa nini Bunge lilipitisha Sh753 bilioni wakati likijua wazi kuwa haziwezi kupatikana, Watanzania watapataje huduma za afya?" alihoji Paresso.
Jaji Werema alijibu akisema Azimio la Abuja ni la hiari na hata kama nchi husika ikishindwa kulitekeleza haitapata adhabu yoyote, huku akisisitiza kuwa Serikali haikupata fedha za kufikia malengo ya azimio hilo na kuahidi kuwa kiwango cha fedha kilichobaki kitaongezwa kabla ya mwisho wa mwezi huu.
CHANZO:MWANANCHI