Tuesday, June 17, 2014

USHAHIDI WA SHAHIDI WA MRAMBA WAFUTWA



USHAHIDI WA SHAHIDI WA MRAMBA WAFUTWA
Na Mwene Said, 
wa Globu ya Jamii Mahakamani

MAWAKILI wa utetezi wa Waziri wa Fedha wa zamani, Basil Mramba, wameondoa mahakamani ushahidi wa Kamishna wa zamani wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Felician Busigara, baada ya kuzua mvutano kati ya mawakili wa pande  zote mbili kwamba ushahidi wa shahidi huo ulikuwa wa kitaalamu na siyo dhidi ya mashitaka yaliyopo mahakamani.
Mbali na Mramba, washtakiwa wengine ni Waziri wa Zamani, Nishati na Madini, Daniel Yona na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Gray Mgonja, wote kwa pamoja wanakabiliwa na kesi ya matumizi mabara ya madaraka na kuisababishia serikali hasara ya Sh. bilioni 11.7.
 
Wakili wa utetezi, Peter Swai, alitoa maombi hayo jana mbele ya jopo la mahakimu watatu, likiongozwa na Mwenyekiti, Jaji John Utamwa akisaidiana na Jaji Sam Rumanyika(walioanza kusikiliza kesi hiyo kabla ya kupanda vyeo) na Msajili Saul Kinemela wanaosikiliza kesi hiyo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam.
Awali, Wakili wa Serikali, Shadrack Kimaro, alidai shauri linakuja kwa ajili ya kutolewa uamuzi wa mahakama kuhusu ushahidi wa shahidi huyo na kuendelea na utetezi.
Hata hivyo, Swai aliomba kumuondoa shahidi huyo na ushahidi wake aliuotoa na aliomba mahakama kupanga tarehe nyingine ya kusikiliza ushahidi wa utetezi kwa kuwa hawakuwa na shahidi.  Upande wa Jamhuri haukuwa na pingamizi kuhusu maombi hayo ya upande wa utetezi.
Jaji Utamwa alisema shahidi huyo wa pili wa utetezi ushahidi wake unaondolewa na kwamba ombi la kuahirishwa linakubaliwa.
Kesi hiyo iliahirishwa hadi Julai 17 na Agosti 15, mwaka huu itakapotajwa na itaendelea kusikilizwa ushahidi wa utetezi Agosti 21, mwaka huu.